MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amekagua shamba la mfano la korosho lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo Kijiji cha Masigati, Halmashauri ya wilaya Manyoni mkoani Singida na kueleza kuwa linaendelea vizuri.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba hilo Novemba 12, 2019 wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua shamba hilo Dkt. Nchimbi alisema kuwa linaendelea vizuri na linaleta matumaini makubwa.
“Hivi sasa mabibo yameanza kuanguka na watu wanayaokota ni dalili nzuri ya maendeleo ya shamba letu na kazi inayoendelea katika shamba hili ni kufanya usafi tayari kwa msimu huu” alisema Nchimbi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, akionesha mabibo aliyoyaokota kwenye shamba la mfano la korosho lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo Kijiji cha Masigati, wilayani Manyoni wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua shamba hilo.
Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa katika msimu huu wanatarajia kupanda ekari zote 12,000 kwani mbegu zipo tayari na zipo za kutosha.
Akizungumza na wananchi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo waliokuwepo katika shamba hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida Oktoba 4, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza Dkt. Nchimbi kwa kulibeba wazo la kuanzisha shamba hilo na kuhakikisha linatimia.
“Nimpongeze Mkuu wa Mkoa kwa kulibeba jambo hili, lakini nikuombe wewe na viongozi wenzako mhamasishe wengine walime zaidi zao hili kwa sababu korosho ni zao kubwa duniani na lina bei nzuri kimataifa,” alisema.
Alisema anatambua kwamba timu ya wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele mkoani Mtwara imeshawasili Manyoni ili kufanya utafiti wa zao hilo na jinsi linavyoweza kuzaa mara mbili kwa mwaka.
“Kwa kawaida, mkorosho mmoja unatoa kilo 40 za korosho kwa msimu mmoja, kwa hiyo kwa misimu miwili mtapata kilo 80. Ninawasii limeni korosho kwa ajili ya watoto wenu ambao wako darasa la pili au la tatu. Mkulima ukianza kuvuna, utaendelea kuvuna kwa miaka 20 mfululizo na kwa hiyo hao watoto hawatahitaji kulipiwa ada wakiwa chuo kikuu sababu korosho itakuwa inawalipia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakulima wanaolima zao hilo wilayani Manyoni, waunde Ushirika wao ambao utawasaidia kuagiza dawa kwa pamoja ama kuuza kwa pamoja.
Hivyo, alimwagiza Afisa Ushirika wa Wilaya hiyo, Yusta Philipo ahakikishe anasimamia jambo hilo kuanzia sasa.
Akitoa taarifa juu ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Kanda ya Kati, Ray Mtangi alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa kilimo cha korosho unajumuisha mashamba makubwa mawili ambapo shamba la Misigati lina ukubwa wa ekari 7,000 na lile la Mikwese lenye ukubwa wa ekari 5,000.
Alisema watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifika shambani hapo ili wajifunze mbinu mpya za kuzalisha korosho kwenye maeneo yao. “Wiki mbili zilizopita, Mheshimiwa Spika na madiwani wa Kongwa walipita hapa ili kujifunza zao hili,” alisema.
Pia alisema Halmashuri yao imetenga eneo la ujenzi wa viwanda na kwamba hadi sasa wanazo ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua shamba hilo na kujionea hali halisi ya shambani ikoje. Pia alioneshwa mabibo na korosho ambazo zimevunwa kutoka kwenye shamba hilo la mfano, kutoka
kwenye mashamba ya wakulima ambao walipanda miche tangu januari mwaka jana.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (kulia) akiwa na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Aderaide Rweikiza wakiokota mabibo katika shamba hilo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.