Serikali imesema inaendelea na mchakato wa kufungua miundombinu mbalimbali ikiwemo njia ya reli kutoka Manyoni hadi Singida ili kusaidia kukuza uchumi na kurahisisha mawasiliano baina ya Mkoa huo na maeneo mengine ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 30.10.2022 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani katika ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Syprian Hilinti wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kati, hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.
Serukamba amesema mchakato huo unaendelea kutokana na maombi yaliyofanywa awali na Kanisa hilo ambapo Serikali ya mkoa imewasiliana na Shirika la reli TRC ambapo bado wanaendelea tathmini za kufungua njia hiyo.
Akiendelea na hotuba RC Serukamba amesema ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa Mkoani hapa upo katika mpango wa Serikali ambapo Mkoa ulipokea maelekezo ya kubainisha eneo la uwanja utakapojengwa.
Hata hivyo ilibainika kwamba eneo la uwanja wa ndege wa sasa limevamiwa na kujengwa nyumba za makazi jambo ambalo linaunyima sifa uwanja huo kutengenezwa kwa hadhi na kiwango cha kisasa alieleza Serukamba.
"Eneo la pili lililobainishwa na kutengewa Kijiji cha Manga linahitaji malipo makubwa ya fidia ili wananchi waliomo ndani ya eneo hilo wapishe kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege" alieleza RC Serukamba
Aidha RC Serukamba amefafanua kwamba barabara ya Singida – Hydom - Mbulu ipo kwenye mpango na utekelezaji wake umeanza ambapo kipande cha Singida - Ilongero - Hydom chenye urefu wa KM 93.3 kazi ya upembuzi yakinifu na maandalizi ya kutangaza zabuni zinaendelea na uthamini katika barabara hiyo umekwisha fanyika.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.