Serikali ya Mkoa wa Singida imesema haitamvumilia mtu yeyote atakayefanya shughuli za kilimo, ufugaji au ujenzi kwenye hifadhi ya msitu wa Mkola uliopo kata ya Mgori Wilaya ya Singida vijijini kwa kuwa uharibifu uliofanyika eneo hilo una athari endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba leo wakati alipotembelea eneo la msitu kwa lengo la kujionea uharibifu uliofanywa na wananchi ambao wamekata miti na kufungua mashamba huku wengine wakianzisha makazi na kufanya shughuli za ufugaji katika msitu huo.
Akiongea na wananchi hao wa Kijiji cha Mkola na Msikii ambao ndio wamiliki wa msitu huo RC Serukamba aliamuru kukamatwa kwa watu watano wakiume wakiwa wanne na mwanamke mmoja ambao walifyeka miti inayokadiriwa kufikia 8,000 iliyopandwa na Serikali mwaka jana na wakafungua mashamba ambapo yamelimwa alizeti kwa sasa.
Akiwa katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Kijiji hicho alitaja majina ya wakulima waliovamia msitu huo na kutoa vitisho kwa viongozi wa Kijiji wakidai kwamba hawana maeneo mengine ya kuendesha shughuli zao.
Watuhumiwa hao watano kati ya wanane walikamatwa na Jeshi la Polisi huku wengine wakiendelea kusakwa ili wafikishwe Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kijiji cha Msikii wametakiwa tarehe 12.5.2023 kufikisha majina ya watu wote wanaolima katika maeneo hayo kwakuwa ndio wanao tuhumiwa kukaidi amri ya Serikali.
RC aliwataka Serikali za vijiji kutumia Sheria na taratibu kuhakikisha msitu huo unalindwa kwa gharama yeyote bila kumuonea mtu kwa kuwa kulima maeneo ya mlimani kumesababisha watu wengi upande wa Kijiji cha Mkola kupoteza makazi yao kwa kupata mafuriko.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskas Muragili amesema msitu huo wenye hekta 1393.6 una umuhimu mkubwa katika utunzaji wa mazingira na Vijiji hivyo viliwahi kutoa Milioni 17 kwa ajili ya utunzaji wa msitu huo hivyo lazima utunzwe.
Alisema mwaka juzi walishirikiana na Vijiji hivyo wakapanda miti 6,000 na mwakajana wakapanda tena miti 8,000 lakini inashangaza kuona miti imekatwa yote na mingine imeliwa na mifungo jambo ambalo amesema Serikali haitalifumbia macho.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.