Serikali imedhamiria kuwaunganisha wakulima wakubwa wa mazao ya chakula wa kata tano za Wilaya ya Iramba kwa kujenga daraja na makaravati manne katika barabara yenye urefu wa kilomita 38.6 yatakayo gharimu shilingi bilioni 4.1.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Mto Mtoa na makaravati katika barabara ya shelui-Mtoa-Urughu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Amour Hamad Amour amesema serikali imedhamiria kuwaunganisha wananchi ili wazalishe mazao, waanzishe viwanda kisha kusafirisha bidhaa.
Amour amesema kwakuwa barabara hiyo inahudumia wananchi wa kata za Shelui, Mtoa, Mtekente, Urughu na Ndago wananchi wa maeneo hayo watumie fursa ya kuwa na barabara nzuri kwa kutengeneza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na kisha kusafirisha bidhaa na sio mazao kama mali ghafi.
Amesema kwa kufanya hivyo wakulima wa mazao wataweza kujiongeza kipato chao kwa kuwa hawatapunjwa kwa kuuzwa mali ghafi ambayo hupelekwa kwenye viwanda vya nchi nyingine hivyo barabara hiyo iwe hamasa kwao kuzalisha kwa wingi pamoja na kuanzisha viwanda kwa wingi.
Mradi huo wa barabara na makaravati unatekelezwa kupitia mpango wa kuondoa vikwazo kwenye barabara za vijijini, mpango unaofadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa kushirkiana na serikali za Uingereza na Ireland Kaskazini.
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja na makaravati hayo kutawezesha barabara hiyo kupitika kwa kipindi cha mwaka mzima na hivyo kuwanufaisha wakazi elfu 79 wa kata hizo pamoja na kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo lenye shule za msingi 29, shule za sekondari 6, zahanati 7 na kituo cha afya kimoja.
Wakati huo huo Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Amour Hamad Amour amezindua mradi wa ghala la kuhifadhia chakula katika kijiji cha Nselembwe ambalo litakuwa likihudumia jamii ya kata za Ulemo,Mgongo, Ntwike, Shelui na Mtoa.
Akifungua ghala hilo Amour amesema kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu ni shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya taifa hivyo ujenzi wa ghala ili kuhifadhi mazao unasaidia wananchi kutoyauza ovyo mazao na kuyahifadhi mahali salama kabla ya kuyachakata kuwa bidhaa.
Amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 350 utaweza kuwasaidia wananchi kuhifadhi mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwa na kauli moja juu ya bei ya mazao pia watakua na uhakika wa mazao.
Amour amewasisitiza wananchi wa kata hizo kuzalisha kwa wingi kwa kuwa sasa wana uhakika wa sehemu salama ya kutunzia mazao yao ili wasishawishike kuyauza kwa bei ndogo.
Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilayani Iramba umetembelea miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 huku ukipitia miradi 6 na kuona shughuli 5 katika vijiji 10 na tarafa 4 katika umbali wa km 119.1.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.