Uongozi wa Kijiji cha Yulansoni katika Kata ya Kinyangiri Wilayani Mkalama Mkoani Singida wameagizwa kuwarejeshea wakulima mashamba wanayogombania kwa kuwa hawana vielelezo vya kutosha vinavyoonesha kuwa waliwakodishia wananchi hao mashamba hayo kwa mikataba.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo baada ya kukutana na viongozi na wazee wa Kijiji hicho pamoja na uongozi wa Wilaya ya Mkalama.
Amesema yupo mwananchi ambaye ni mjane anayelalamikia kuzuiliwa kutumia ardhi yake ambayo alifyeka wakati likiwa shamba pori toka mwaka 1988 lenye jumla ya ekari 65 ambapo viongozi wa kijiji hicho walidai kwamba walimkodishia kwa mkataba wa miaka nane (8) jambo ambalo RC Serukamba alitaka Ofisi ya Kijiji kuwasilisha muhutasari wa vikao na mkataba wa makubaliano hayo.
Aidha, Kijiji kiliwasilisha bàadhi ya nyaraka ambazo baadhi zinaonesha maandishi ambayo yanamtaja mjane huyo badala ya mume wake ambaye ndio alikuwa mmiliki wa shamba hilo, ambapo RC Serukamba alisoma nyaraka hizo na kuonekana ziliandikwa mwaka 2005 badala ya 1998 ambapo marehemu ndipo alipofyeka shamba hilo.
Hata hivyo upande wa mlalamikaji uliendelea kudai kwamba Kijiji hicho kinahitaji shamba hilo ambalo sio mali yake ili kulikodisha ambapo tayari walishachukua fedha ambapo wanatakiwa akimkabidhi shamba au kurudishiwa fedha zake.
Kwa upande wake OCD wa Mkalama alikiri kwamba walipata malalamiko ya mwananchi huyo dhidi ya Kijiji cha Yulansoni ambapo walibaini mwananchi huyo aliachiwa shamba hilo na marehemu mume wake ambaye naye alipata kwa kufyeka pori huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Mesos akieleza kwamba aliwakutanisha mdai na mdaiwa ambapo maelezo ya wote wawili yanabainisha kwamba mwananchi huyo anamiliki eneo hilo.
Kutokana na maelezo hayo RC Serukamba aliwataka viongozi hao kuliachia shamba hilo kwa mwananchi huyo aweze kuendeleza shughuli zake za kilimo na kama hawajaridhishwa na uamuzi huo waende Mahakamani.
Naye Miwani wa Kata ya Kinyangiri Emanuel Kabea alimuomba RC kutembelea eneo lingine ambalo na lenyewe lina migogoro na Kijiji ambapo mwananchi aliyefahamika kwa jina la Edward Mnoma alichukua shamba hilo lenye ukubwa wa ekeri Mia moja (100) ambalo lilikuwa ni eneo la hifadhi ya Msitu wa Kijiji na akaliuza ambapo kwa sasa limebaki ekari 30 tu.
Aidha Diwani huyo amemuomba RC kutembelea eneo hilo na kuona kama ekari hizo 30 zilizopo zinaweza kubaki katika umiliki wa Kijiji hicho jambo ambalo RC Serukamba aliahidi kutembelea eneo hilo baada ya wiki ijayo kupita.
Wakimalizia mjadala huo viongozi hao wa kijiji walimueleza Mkuu wa Mkoa huyo kwamba watarejesha shamba hilo kwa mlalamikaji huku wakijipanga ili kwenda kutafuta haki yao Mahakamani.
Mjadala huo ni muendelezo wa zoezi la utatuzi wa kero za Wananchi zilizotokana na ziara zake katika Halmashauri zote za Mkoa huo ambapo aliwasikiliza wananchi kwa kipindi cha Siku nne mfululizo.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.