Walimu wa shule za Serikali Mkoani Singida wametakiwa kuhakikisha wanafuta daraja la sifuri na daraja la nne kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwashirikisha wazazi na wanafunzi wenyewe.
Akiongea katika kikao kazi kilichowakutanisha Walimu wa shule za msingi, sekondari na wadhibiti ubora uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa RC Mission uliopo mjini Singida.
RC Serukamba amesema uondoaji wa madaraja hayo ya elimu utawezekana kwa kuacha uzembe, kuwahi kazini na kuwa na tabia ya kupata mrejesho baada ya kufundisha huku akiwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula mashuleni.
Hata hivyo amewataka Maafisa elimu wa kata kuhakikisha wanatembelea mashule na kuhakikisha kila mwalimu anatimiza majukumu yake huku akiwakumbusha wadhibiti ubora kutowadhibiti walimu pekee badala yake waangalie changamoto zinazo wakabili walimu.
Aidha amewakumbusha walimu kahakikisha kwamba katika Mkoa wa Singida hakutakuwa na Mwanafunzi atakayemaliza darasa la Saba bila kujua kusoma na kuandika.
Katika kuboresha Elimu RC Serukamba ameeleza nia yake ya kutaka kuanzisha mashindano kwa Shule za Sekondari ambapo shule ambayo haitapata daraja sifuri na daraja la nne watapata zawadi itakayo gawanywa kwa walimu wote wa shule husika.
"Umefika wakati sasa wadhibiti ubora kuhakikisha tunapata elimu bora kwa kuwa Serikali imeshawekeza vya kutosha katika majengo na miundombinu ya shule, umefika wakati Serikali kuwekeza katika ujuzi ili kuleta ubobezi katika masomo yanayofundisha" alieleza RC Serukamba.
Hata hivyo amewataka walimu kuendeleza juhudi na utamaduni wa kusoma vitabu badala ya kutumia mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko amesema Mkoa una jumla ya Walimu 7492 ambapo wa shule ya msingi ni 5166 na Sekondari ni Walimu 2326.
Amesema uwepo wa walimu hao kumesababisha kuanza kuboresha elimu ambapo amesema kwa kidato cha sita ambapo ufaulu umefikia daraja la kwanza na kwa wanafunzi wa darasa la nne ameeleza kwamba waliofanya mtihani ni asilimia 93 na waliofaulu ni asilimia 82.
Hata hivyo RAS amesema katika zoezi la kuboresha elimu mkoani hapo tayari wameanzisha mkakati maalum ambapo utaboresha mahudhurio ya Walimu na Wanafunzi, ujenzi wa miundombinu na kuboresha uwajibikaji.
Aidha Mwaluko amesema tayari wameshaanza mafunzo ya Walimu ambapo jumla ya Walimu 1972 kati ya 7000 wameaanza kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Awali na Msingi TAMISEMI Suzan Nusu ameagiza kuendelea kutolewa kwa Mafunzo endelevu ya walimu kazini (Mewaka) ndani ya shule ili kujengeana uwezo na kuboresha Elimu na ufundishaji.
Mkutano huo ulihudhuriwa na jumla ya walimu 1956 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Singida na kuhusisha walimu wa shule ya msingi, sekondari, Tume ya Utumishi wa walimu na wadhibiti ubora.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.