Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida kwa kipindi cha Januari 2023 hadi Juni 2023 kwa Halmashauri Kuu ya chama hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti Martha Mlata.
Taarifa hiyo ameitoa leo (tarehe 28/7/2023) katika ukumbi wa chuo cha Uhasibu kilichopo Singida mjini ambapo amesema Mkoa wa Singida umetekeleza ahadi mbalimbali katika sekta za uzalishaji, uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuboresha miundombinu na kupanga matumizi bora ya ardhi.
Aidha amesema utoaji huduma bora za kijamii zimetolewa zinazojumuisha Elimu, Afya na Maji, kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, masuala ya utawala bora na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na makazi ya wafanyakazi.
Akizungumzia hali ya uchumi ameeleza kwamba, asilimia 80 ya wananchi wa Mkoa wa Singida wanajihusisha na shughuli za sekta ya Kilimo (Kilimo, Ufugaji, Uvuvi). Aidha, Usalama ndani ya Mkoa umeimarika na kuwezesha wananchi kutekeleza majukumu yao ya kiuchumi na kijamii kwa amani na utulivu.
Ameeleza kwamba hali hiyo imewezesha hali ya uchumi kuwa na mafanikio katika kukua kwa Pato la Mkoa (GDP) kutoka Shilingi Trilioni 2.8 mwaka 2020 hadi kufikia Shilingi Trilioni 3.019 mwaka 2021. Kuongezeka kwa Mpango na Bajeti ya Mkoa kutoka Sh. 199,170,767,000 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh 230,988,225,000 ambayo mkoa imekadiria kutumia kwa mwaka 2023/2024.
Amefafanua kuwa kukua kwa Pato la wastani la kila mtu kwa Mkoa wa Singida kutoka Sh 1,651,785 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi 1,721,195 mwaka 2021.
Serukamba amesema ili kuwawezesha Wananchi kiuchumi, Serikali imesimamia sheria ya fedha za Serikali za Mitaa katika kuwezesha vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu kupata mikopo kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri.
Aidha, amesema fedha za mapato ya ndani ya asilimia kumi jumla ya Shilingi 636,658,546.38 sawa na 45.5% kati ya shilingi 1,398,543,620.21 zimetolewa katika kipindi cha Januari 2023 hadi Juni 2023 kwa Vikundi 134 vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu ambapo Vikundi 49 vya Vijana vimepewa Shilingi 250,655,767.00
Amesema Vikundi 69 vya Wanawake vimepewa Shilingi 326,107,503.26 na Vikundi vya Watu wenye Ulemavu 16 vimepewa Shilingi 59,895,276.12
Akizungumzia uwekezaji Mkuu wa Mkoa huo amesema jumla dolla za kimarekani million 40 zimewekezwa Halmasahuri ya Ikungi katika mgodi wa Shanta wenye eneo la kilomita za mraba 29 la uchimbaji ambapo shughuli za maandalizi ya uchimbaji zinategemea kuanza mwezi Agosti 2023.
Aidha katika Halmashauri ya Iramba uwekezaji wenye thamani ya Tshs 1,165,835,154,173.54 wa uchimbaji wa madini umewekezwa na wawekezaji 3. Jumla ya ekari 59,670 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji kilimo cha alizeti na korosho katika Halmashauri ya Ikungi, Mkalama na itigi
Kwa upande wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), utekelezaji wa mpango wa kunusuru Kaya maskini katika Mkoa wa Singida umefanyika ambapo jumla ya Shilingi 9,249,051,072/= zililipwa kama ruzuku kwa walengwa 134,275 katika Vijiji 502 vinavyonufaika na mpango kufikia mwezi June, 2023.
Aidha katika kaya za walengwa hao jumla ya watoto 18,465 walio chini ya Miaka 5 pamoja na watoto 59,230 wanaosoma shule za Msingi na Sekondari wamenufaika.
Akizungumzia Kilimo amesema, Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023, tani 726,771.3 (55.8%) za mazao ya chakula zilizalishwa kati ya lengo la tani 1,300,232.7 na mazao ya biashara tani 342,405.7 (49.3%) zilizalishwa kati ya tani 843,595.
Amefafanua kuwa mazao ya chakula yanayozalishwa ni pamoja na mtama, uwele, viazi vitamu, mihogo, mahindi na jamii ya mikunde na mazao ya biashara yanayojumuisha alizeti, korosho, pamba, ufuta, vitunguu, choroko na dengu.
Amesema mahitaji ya chakula kutokana kulingana na idadi ya watu 2,008,058 kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya 2022 ni Tani 542,175.7 za chakula ambazo kulingana na takwimu zilizotolewa hadi kufikia mwezi Juni Mkoa una ziada ya chakula Tani 184,595.6 za mazao ya chakula.
Takwimu zote za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara zitakamilika ifikapo Agosti 15, 2023 ambapo mazao yote yatakuwa yamevunwa mashambani.
Hata hivyo ameeleza kwamba Mkoa umejipanga katika kufanikisha kilimo cha mazao ya kimkakati katika zao la Korosho ambapo lengo la kilimo katika msimu wa 2022/23 lilikuwa kuvuna jumla ya tani 1,721.4 ambapo mavuno yaliyopatikamna ni tani 994.4 Kati ya tani zilizovunwa tani 36 ziliuzwa kwa bei ya Tshs. 1610 kwa kilo na kuzalisha pato la Tshs. 57,960,000 kwa wakulima.
Halmashauri zimeendelea kuzalisha miche ya korosho ambapo jumla ya miche 218,868 imezalishwa na kupewa wakulima.
Kwa upande wa kilimo cha Alizeti amesema kwa mwaka 2022/23, jumla ya tani 230,129.5 (44.7%) zilizalishwa kati ya tani 511,500.11 na Vitunguu kwa msimu wa mwaka 2022/23, eneo liliolimwa vitunguu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida ni hekta 18,147 ambapo mavuno yalikuwa tani 53,599.7
Serukamba amesema katika kilimo cha Umwagiliaji Elimu imetolewa kwa wakulima 2,350 kati ya 7,039 kuhusu kilimo bora na utunzaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu tisa (9) za Itagata-Itigi, Msemembo, Udimaa, Ngaiti, Chikuyu, Maweni, Mtiwe (Manyoni), Mang’onyi (Ikungi) na Masimba (Iramba). Aidha jumla ya Tshs 5,000,000.00 zilitumika kutekeleza shughuli hii.
Akizungumzia Mifugo amesema udhibiti wa magonjwa ya mifugo kwa njia ya chanjo na uogeshaji umefanyika. Jumla ya N’gombe 506,971 mbuzi 60,741, kondoo 32,426 mbwa 31,926 wameogeshwa pamoja na uchanjaji wa jumla ya n’gombe 84,120, mbuzi na kondoo 21,724, kuku 456,351, na mbwa 1,996 dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Katika Sekya ya Msitu na Maliasili amesema jumla ya miti 6,500,000 imepandwa katika kipindi cha mvua sawa na asilimia 61.9 ya utekelezaji wa lengo la kupanda miti 10,500,000 kwa mwaka. Mkoa umeendelea kutunza Mapori ya akiba ya Muhesi, Kizigo na Rungwa yenye ukubwa wa KM za mraba 17,300.
Akizungumzia Sekta ya Viwanda amesema utekelezaji uliofanyika katika jitihada za kuongeza viwanda hadi kufikia Juni, 2023 ni kuanzishwa viwanda 118 vinavyojumuisha viwanda vidogo sana 64, vidogo 45 na viwanda vya kati 9. Uhamasishaji katika uwekezaji wa viwanda ni pamoja na kutangaza fursa zilizoainishwa katika Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa.
Kwa upande wa Madini amesema jumla ya leseni 195 sawa na 97.5% ya lengo la leseni 200 za uchimbaji mdogo wa madini zimetolewa kwa wawekezaji binafsi. Mafunzo yametolewa kwa wachimbaji wadogo 2,000 sawa na 100% ya lengo kuhusu uchimbaji wenye tija.
Kwa upande wa Sekta ya Miundombinu amesema Wakara wa barabara TANROAD wameendelea kufanya matengenezo ya kawaida, matengenezo ya vipindi maalum, matengenezo ya sehemu korofi, na matengenezo ya madaraja ambapo hali ya barabara imeendelea kuimarika na kuridhisha ambapo 70% zina hali nzuri, 26.2 zina hali ya wastani na 3.6 zina hali mbaya. Barabara zenye hali mbaya ni zile zilizopandishwa kutoka barabara za Wilaya ili zihudumiwe katika barabara za Mkoa.
Kwa upande wa TARURA mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Ujenzi wa km 5.59 za barabara za lami kati ya km 6.03, Matengenezo ya kawaida km 433.65 kati ya km 431.42, Matengenezo ya muda maalumu km 452.05 kati ya km 455.34 na sehemu korofi km 102.38 kati ya km 98.74.
Ujenzi wa vivuko umefanyika kwa 93.70% na mifereji kwa 108.90% kulingana na malengo yaliyowekwa.
Aidha Kiasi cha shilingi 18,692,650,282.62 zimetumika kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara/vivuko pamoja na usimamizi na ufuatiliaji.
Kwa upande wa Umeme amesema Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441 ambapo Vijiji vyenye umeme hadi kufikia mwezi Juni 2023 ni 341 na Vijiji 100 vilivyobaki vitakamilika kupelekewa umeme ifikapo Desemba 2023.
Aidha katika Mkoa wa Singida, Jumla ya miradi kabambe mitano (5) ya kusambaza umeme Vijijini inatekelezwa ambapo miradi miwili (2) ipo katika hatua ya utekelezaji na miradi mitatu (3) ipo katika hatua ya awali za utekelezaji.
Akizungumzia Elimu amesema, Mkoa wa Singida mwaka 2023 uliandikisha wanafunzi wa Elimu ya Awali 54,603 wakiwemo Wavulana 27,756 na Wasichana 26,847 sawa na asilimia 99.01 ya lengo la unadikishaji.
Mkoa wa Singida uliandikisha wanafunzi wa darasa la Kwanza 57,667 wakiwemo wavulana 29,211 na wasichana 28,456 sawa na asilimia 102. Mwaka 2023, Mkoa ulidahili wanafunzi wa Kidato cha Kwanza wapatao 28,153 kati ya wanafunzi 32,218 waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza sawa na asilimia 87.38 (Wavulana 12,844 na Wasichana 15,309).
Amefafanua kuwa, jumla ya Watahiniwa 42,538 walifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba (PSLE 2022) ambapo watahiniwa 32,252 (7.5%) walifaulu. Jumla ya wanafunzi 64,403 walifanya mtihani wa upimaji wa darasa la nne ambapo wanafunzi 47,999 (80.6%) walipata alama za ufaulu.
Amesema jumla ya wanafunzi 42,538 walifanya Mtihani wa darasa la Saba ambapo Wanafunzi 32,252 walifaulu sawa na asilimia 75. Jumla ya wanafunzi 17,717 walifanya Mtihani wa kidato cha Pili ambapo Wanafunzi 14,540 walifaulu sawa na asilimia 82.06
Ameongeza kuwa jumla ya wanafunzi 15,057 walifanya mtihani wa upimaji Kidato cha Nne ambapo wanafunzi 13,151 (87.3%) walifaulu. Jumla ya wanafunzi 1,612 walifanya mtihani wa upimaji Kidato cha Sita ambapo wanafunzi 1,612 (100%) walifaulu.
Katika utekelezaji wa Miradi ya Elimu kupitia Mradi wa BOOST amesema, Mkoa wa Singida ulipokea kiasi cha shilingi 9,024,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya 12, madarasa ya mfano Elimu ya Awali 14 kwa Elimu ya Awali, matundu 115 ya vyoo, nyumba 2 za Walimu, madarasa 106 shule za msingi, madarasa 161 shule mpya, Ukarabati wa Shule Kongwe 1 na Majengo ya Utawala 12.
Kupitia Fedha za Serikali Kuu, Mkoa ulipokea shilingi 4,566,400,000 kwa ajili ujenzi wa madarasa 46, matundu 581 ya vyoo, nyumba 20 za walimu, ukamilishaji wa vyumba vya madarsa 101, Uzio kwa ajili mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalum-shule 3, na Ujenzi wa Shule mpya 1.
Kupitia Mradi wa SRWSS, Mkoa wa Singida ulipokea shilingi 1,158,219,746.76 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 507 ya vyoo, miundombinu ya kunawia mikono, matanki ya maji safi katika Shule za Msingi. Miradi hii sehemu kubwa imekamilika na mingine ipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji.
Kupitia Mradi wa TEA, Mkoa ulipokea fedha shilingi 446,586,112 kutoka TEA kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, Ofisi, Nyumba na matundu ya vyoo katika shule za Msingi. Mkoa ulipokea kiasi cha shilingi 3,712,800,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Shule za Sekondari.
Kupitia Mradi wa SEQUIP, Mkoa ulipokea kiasi cha shilingi 6,223,805,008 kwa ajili ya ujenzi mindombinu ya Kidato cha Tano, Ujenzi wa Shule 8 za Kata na Umaliziaji wa ujenzi wa Shule 1 (Solya) Kitaifa ya Wasichana.
Kupitia Mradi wa Barric, Mkoa wa Singida ulipangiwa shilingi 223,800,000 kwa ajili ya upanuzi wa Shule ya Sekondari Tumaini iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Iramba. Miundombinu inayojengwa ni madarasa 4, Bweni 1 na matundu 4 ya vyoo. Hatua ya ujenzi wa mindombinu.
Katika sekta ya Afya Mkoa umeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika Vituo 259 vya kutolea huduma za afya ikijumuisha Hospitali 11, Vituo vya afya 22, Zahanati 220 na Kliniki 6. Utekelezaji kufikia Juni 2023 ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Mkalama na Singida DC kwa majengo ya wodi na upasuaji.
Aidha Ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ya Itigi na Ikungi pamoja na ukarabati wa Hospitali ya Manyoni ambazo zote kwa ujumla zimepokea kiasi cha Tshs 2,250,000,000. Ukamilishaji wa Zahanati 11 kwa thamani ya shilingi 750,000,000.00 ambapo kila Zahanati ilipatiwa Tshs 50,000,000 kwa mchanganuo Manyoni (2), Ikungi (2), Mkalama (2), Iramba (2) Itigi (2), Singida MC (1) na singida DC (1).
Ukamilishaji wa vituo vya Afya 12 kupitia fedha za Tozo zilizopokelewa Novemba, 2021 ambapo kila kituo kilipokea kiasi cha shilingi Milioni 500 kwa ajili ya majengo ya upasuaji , wodi ya wazazi, kufulia na njia ya kutembea kwa miguu.
Ukamilishaji wa majengo matatu (3) ya dharura (EMD) kwenye Hospital 3 za Wilaya ya Iramba, Manyoni na Mkalama, majengo 2 ya kuhudumia wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali za Wilaya za Iramba na Singida ambayo yapo katika hatua za ukamilishaji.
Mkoa wa Singida kupitia Mkuu wa Mkoa Ndg. Peter Joseph Serukamba anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia Mkoa wa Singida fedha nyingi za maendeleo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Kilimo, Barabara, Nishati, Maji, Uwezeshaji wananchi kiuchumi ambazo zinagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania katika Mkoa wa Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.