Mkoa wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan Mkoa huu umepewa Sh.bilioni 210 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara.
Amesema hayo (Septemba 10, 2023) wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi wa kampuni ya Henan High Way Engeneering Group mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka -Ndago hadi Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 ambayo Serikali imetoa Sh.bilioni 88 kwa ajili kuijenga kwa kiwango cha lami.
Serukamba amesema pia katika kipindi hicho Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) Mkoa wa Singida umepatiwa Sh.bilioni 34 ambapo miradi kadhaa imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82 lililojengwa kwa Sh.bilioni 32, daraja a Msingi mita 100 kwa Sh.bilioni 11.9 na ujenzi wa barabara ya Itigi yenye urefu wa kilometa 10 kwa Sh.bilioni 8.9.
Aliongeza kuwa barabara ya Itigi kwenda Mbeya zimetengwa Sh.bilioni 60 na kwamba barabara zote zinazoendelea kujengwa mkoani hapa zikikamilika Singida itakuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao mbalimbali ambayo yatafikishwa kwa urahisi kwenye masoko yaliyopo ndani na nje ya mkoa.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Serukamba amesema Mkoa wa Singida umepanga katika msimu wa kilimo mwaka huu kulima ekari milioni moja za alizeti kutoka ekari 681,000 zilizolimwa msimu uliopita lengo ni kuhakikisha mafuta ya kula ya kulisha nchi nzima yawe yanatoka Singida.
"Kuna miradi 12 ya mabonde ya umwagiliaji kwa Mkoa wa Singida ambayo ujenzi wake upo katika hatua mbalimbali, tukimaliza miradi ya umwagiliaji yote vitunguu vyote vya nchi hii ufuta, dengu, pamba, korosho, mahindi, mafuta ya alizeti vitatoke Singida,"alisema Serukamba..
Kuhusu mbolea, Serukamba amesema maelekezo ya Wizara ya Kilimo yalishatolewa ambapo ifikapo Septemba 20, mwaka huu mbolea itakuwa imefika kila Wilaya.
"Mwaka huu niwahakikishie wana Singida hakuna kijiji ambacho mbolea haitafika, kazi imeanza na maafisa kilimo safari hii sitawaachia tutasimamia mimi na ma-DC (Wakuu wa Wilaya) wangu kuhakikisha mbolea na mbegu inafika kwa wakati ili watu wasipate sababu, nataka safari hii tuongeze uzalishaji wa mazao," alisema.
Serukamba akizungumzia maji, alisema katika vijiji 441 vilivyopo katika mkoa huu asilimja 66 vinapata huduma ya maji na mjini upatikanaji wa maji ni asilimia 85 na malengo ifikapo 2025 upatikanaji wa maji vijijini itafikia asilimia 80 na mjini asilimia 100.
Kuhusu umeme amesema vijiji 341 kati ya 441 vilivyopo mkoani hapa vimepata umeme na vijiji 100 vilivyobaki wakandarasi wapo kazi wakiendelea na kazi na ni matumaini ifikapo mwakani vijiji vyote vitakuwa vimefikiwa na umeme.
"Sisi wanaSingida tuna deni kwa Rais Samia Suluhu Hassan na tuna shauku kubwa sana kumlipa deni na deni hili tutaanza kulilipa 2024 na kumalizia 2025, wanaSingida wanamwelewa sana Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Serukamba.
mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.