MKE wa Waziri Mkuu Mstaafu,Tunu Pinda ameitaka ,Serikali, wadau wa maendeleo, taasisi za Serikali na wananchi kwa ujumla mkoani Singida kuchukua hatua za makusudi kushughulikia masuala ya ubaguzi wa kijinsia na uonevu wanavyofanyiwa Wanawake.
Wito huo ameutoa leo Machi 8, 2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa wilayani Ikungi mkoani hapa ikiwa na kauli mbiu ya wekeza kwa mwanamke kuharakisha maemdeleo ya taifa na ustawi wa jamii.Pinda alisema Tanzania inaunga mkono jitihada za kimataifa za kukuza usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kujielekeza katika utekelezaji wa mikakati ya kufikia kizazi chenye usawa.
Alisema Serikali katika kutekeleza hilo imezindua Kamati ya ushauri ya Kitaifa ya utekelezaji wa ahadi za nchi kuhusu kizazi chenye usawa uliofanyika tarehe 16 Disemba, 2021 Jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikuwa rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Alisema kuanzishwa kwa kamati hiyo ni jitihada za Serikali katika kutoa msukumo wa utekelezaji wa masuala ya haki na usawa kwa wanawake na wanaume.
Nachukua nafasi hii kumpongeza Mwanamama, Amiri Jeshi Mkuu, na Raisi Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uhodari wake wa kufanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko kila sekta nchini katika kuleta miradi ya maendeleo endelevu, kila mkoa hadi wilaya, kata na hata mtaa na sisi wanawake tukiwa ni wanufaaika wakubwa wa Maendeleo haya,"alisema Pinda.
Aidha, aliwapongeza wanawake wote nchini na hususani wanawake wa Mkoa wa Singida kwa upambanaji, wajasiri na hodari kwa kuchapa kazi.
Alisema lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za kimataifa, kikanda na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wanawake.
Alisema kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa haki za wanawake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.
"Kuadhimisha siku ya wanawake duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo pamoja na kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na serikali na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla," alisema Pinda.
Alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inaendana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwekeza kwa wanawake kiuchumi, Kijamii, Kiafya, Elimu, Michezo na Utamadumi.hivyo ni wajibu kwa wanawake kutambua hilo na kumuunga mkono Rais kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuwezesha wanawake,na kuleta mabadiliko kila sekta nchini katika kuleta Miradi ya maendeleo endelevu.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mendeleo Jamii Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu, inayoongozwa na Mwanamama, Doroth Gwajima inadhamini na kuwatambua umuhimu wa wanawake wote na wajasiriamali ni miongoni mwa watu muhimu katika kukuza uchumi wa mtu moja moja na Pato la Taifa.
"Nitoe rai kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kutenga eneo maalumu katika masoko yao kwa ajili ya malezi yaani Day care Center ili kuwezesha wanawake wajasiriamali wenye watoto waweze kupata sehemu maalumu ya kunyonyesha na watoto kupata muda wa kucheza, hali hii itaboresha zaidi malezi na makuzi ya Awali ya Watoto na kuimarisha usalama wao," alisema Pinda.
Kwaupande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amesema siku ya Mwanamke Duniani ni siku ya kutazama na kutafakari juu ya nafasi ya Mwanamke katika suala zima la maendeleo. ni siku ya kujipima na kutathimini namna gani wanawake wamewezeshwa kujitambua na kushirikishwa katika mipango ya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na wanaume.
"Kwa namna ya pekee katika kusheherekea siku hii sisi wanasingida tunataka kumuelezea mwanamke Jasiri muongoza njia, shupavu na mfano bora wa kuigwa sio tu na kila mwanamke bali kila mtanzania bila kujali ni mwanamke au mwanaume. Mwanamke huyo ni: Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan". Amesema RC Serukamba
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.