Mkoa wa Singida umedhamiria kuondoa changamoto ya mimba na ndoa za utotoni kwa mtoto wa kike.
Akizungumza kwenye kikao cha kujadili changamoto ya mimba za utotoni kilichofanyika Wilaya ya Manyoni Katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki hivi karibuni Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge, amesema kuwa serikali itaendelea na juhudi za kuhakikisha haki za mtoto wa kike zinaheshimiwa na kulindwa.
Dkt. Mahenge amesema, serikali itawachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya ukatili, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni Kama sehemu ya kulinda Haki za mtoto
RC. Mahenge amesema, ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, Serikali imejipanga kikamilifu na kwa kuanzia inatoa elimu kwa jamii na kuimarisha mifumo ya upatikanaji haki ili kukabiliana na wahusika watakaothubutu kwa ajili ya kuyaathiri mapambano hayo.
“Ndoa na mimba za utotoni zinatajwa kuwa ni kikwazo kikubwa kwa mtoto wa kike…hali hii inachangiwa zaidi na mila potofu na desturi kwa baadhi ya makabila, ambayo kwa namna moja au nyingine yanakandamiza haki za mtoto wa kike”. Amesema Dkt. Mahenge
Amesema baadhi ya makabila hadi leo hii yanamuona mtoto wa kike ni bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa sokoni baada ya kuvunja ungo, wakati uhalisia mtoto wa kike ni sawa na mtoto wa kiume na anahitaji haki sawa za msingi, ikiwemo elimu.
Katika kukabiliana na janga hilo ndani ya mkoa wa Singida, Dkt. Mahenge amesisitiza kwamba Jeshi la Polisi, Ustawi wa Jamii na vyombo vya habari, vihakikishe vinamtendea haki mtoto wa kike, kwa kutoa elimu sahihi itakayomkoamboa kutoka katika ukatili.
Pia Dk. Mahenge amewaasa Walimu katika shule za msingi, sekondari, watendaji wa vijiji na Kata, kutoa elimu na kuripoti matukio ya ukatili, huku jamii nayo ikitakiwa kuonyesha ushirikiano kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika na mashirika yanayojitolea katika kukabiliana na changamoto hizo.
“Serikali haiwezi kunyamazia tabia hii, pale itakapobainika na tukapata taarifa sahihi, tutachukua hatua mara moja…lakini hayo yote hayatawezekana ikiwa tutafanya wenyewe, tunahitaji wadau wengi zaidi ili tuweze kushirikiana nao, kwa juhudi za pamoja”. Dkt. Mahenge
Aidha Dkt. Mahenge amelishukuru shirika la Compassion Internation Tanzania, kwa kuandaa mkutano huo ili kuweza kushirikiana na serikali na kanisa, katika kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ukatili, kwa lengo la kumkomboa kijana, kutoka kwenye lindi la umasikini, hususani katika mkoa wa Singida.
Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Singida Bi. Shukrani Mbago akizungumza wakati wa kikao
Naye Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Singida Bi. Shukrani Mbago, amesema katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Itigi na Ikungi, takwimu zinaonyesha wasichana 98 waliokuwa shuleni katika kipindi cha januari hadi disemba mwaka jana, walipata mimba
Mbago amefafanua katika kipindi cha mwaka jana (2021) kuanzia januari hadi disemba, jumla ya wasichana 12,000 wa mkoa wa Singida wenye umri chini ya miaka 20, walio nje ya mfumo rasmi wa elimu, walipata ujauzito, hivyo kuathiri ndoto zao za kuwa na maisha bora siku za mbeleni.
Bi. Mbago amesema, mtoto wa kike anapopata mimba akiwa na umri wa chini ya miaka 20, anapata vihatarishi vingi na madhara mengi ya kiafya, hasa wakati wa kujifungua.
Amefafanua kuwa, binti anayejifungua katika umri huo huwa hukosa malenzi ya pamoja kutoka kwa wazazi, jambo ambalo husababisha kuimbe kitakachozaliwa, kukua na kulelewa kinyume na maadili, hivyo kusababish ongezeko la watoto wa mitaani.
Mchungaji wa Kanisa la Aglican - Muhalala wilayani Manyoni Gabriel Masanja akizungumza na waandishi wa habari (hawwapo pichani) mara baada ya kumaliza kikao
Kwa upande wake mchungaji wa Kanisa la Aglican lililopo kijiji cha Muhalala wilayani Manyoni Gabriel Masanja,amesema kati ya visababishi vya ndoa na mimba za utotoni ni migogoro ya kifamilia inayochangia wazazi kutengana, elimu duni ya malezi na jinsi ya kujikinga na kujiepusha na vishawishi.
Mchungaji Masanja alitaja visababishi vingine ni, mila na desturi potofu, utandawazi, mazingira hatarishi, umasikini uliokithiri ndani ya familia hivyo kuwezesha watoto kwenda kujitafutia mali kwa njia zisizokuwa halali, ili kuweza kujikimu kimaisha.
Kutokana na hali hiyo, mchungaji Masanja ameiomba jamii kuhimiza watoto wao kwenda katika nyumba za Ibada kwa ajili ya kupata mafundisho kulingana na imani zao, ili kuimarika katika malezi bora na hivyo kujikwamua kiuchumi katika familia zao.
Kaimu mkurugenzi shirika la Compassion Internatinal Tanzania, Mary Kassanga akizungumza wakati wa kikao
Katika kikao kazi hicho maalumu cha kujadili changamoto za mimba za utotoni kwa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Manyoni na Itigi, kaimu mkurugenzi shirika la Compassion Internatinal Tanzania, Mary Kassanga, ameishukuru serikali ya mkoa wa Singida kuweza kujumuika na shirika lake, katika mapambano hayo.
Kassanga amesema kuwa, ingawa shirika lake ni la kikristo, lakini limejikita katika maendeleo ya mtoto na utetezi wa anayeishi katika mazingira ya umasikini, na huduma hiyo inatekelezwa kupitia ushirika wa makanisa na wadau wengine, ikiwemo serikali.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa, tunahudumia watoto bila kujali dini, kabila au utambulisho wowote, tunatumia mbinu mtambuka kukabiliana na changamoto za maendeleo zinazowakabili watoto kutoka kwenye familia masikini…dhamira yetu ni kuwakomboa watoto katika umasikini,”alisema Kassanga.
Amesema kuwa, hadi sasa shirika lake linafanya kazi na makanisa washirika-wenza katika mikoa 21 ya Tanzania bara kwenye halmashauri zaidi ya 80, huku likitekeleza majukumu yake kwa makanisa zaidi ya 500 na watoto 109,000 wakifadhiliwa na shirika hadi kufikia mwaka wa fedha wa 2021.
Kassanga amefafanua kuwa, mkakati wa shirika kwa mwaka 2021-2022 unalenga zaidi katika kuboresha maisha ya watoto na vija na zaidi ya milioni tano, hasa wale wanaoishi kwenye mazingira magumu ya umasikini zaidi.
Katika kipindi hicho, Kasanga amesema, watalenga zaidi katika kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto, elimu, shughuli za kujiingizia kipato, maji na usafi wa mazingira.
Kassanga amesema, ingawa shirika lake linahudumia watoto 9,233 kwa halmashauri ya wilaya Ikungi, Manyoni, Itigi, Iramba na Singida vijijini, takwimu za shirika kwa januari mwaka huu katika vituo 15 vya maendeleo, kwa Ikungi, Manyoni na Itigi, watoto 57 walipata mimba, hivyo kuathiri maendeleo yao.
Kikao kikiendelea
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kulia) akizungumza na wajasiriamali alipotembelea mabanda.
Picha ya pamoja
MWISHO.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.