Mkoa wa Singida unategemea kuvuna tani 580,000 za alizeti katika msimu wa kilimo wa 2021/22 kulikochagizwa na ukopeshwaji wa mbegu zenye ruzuku ya Serikali kwa wakulima wa zao hilo ambapo uzalishaji unakadiriwa kuongezeka zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na msimu uliopita.
Akitoa kauli hiyo wakati alipotembelea mashamba ya wakulima mbalimbali katika Kata ya Mudida Halmashauri ya Singida Vijijini Mkuu wa mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge amesema wakulima wadogo na wakubwa wameitikia kwa kiasi kikubwa na mbegu walizotumia zimeonesha dalili ya kutoa mavuno mengi.
Mkuu wa mkoa Singida Dkt. Binilith Mahenge wakati akisisitiza jambo wakati alipotembelea mashamba ya wakulima mbalimbali katika Kata ya Mudida Halmashauri ya Singida Vijijini Machi 23, 2022
Hata hivyo RC Mahenge amewataka Maafisa Kilimo mkoani hapo kuhakikisha wanaendelea kuwatembelea wakulima na kuwashauri namna ya kutumia dawa kuzuia visumbufu vya mimea vinavoweza kutokea kutokana na mvua kuendelea kunyesha.
Aidha Dkt. Mahenge akamuagiza Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na uzalishaji Beatus Choaji kuitisha mkutano wa wadau wa alizeti ili kuanza kutafuta soko la uhakika la wakulima ili wasije kupata hasara wakati wa mavuno.
Hata hivyo Dkt. Mahenge akabainisha kwamba kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la alizeti mkoani hapo kuna kila dalili kwamba uagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi utaanza kupungua kutokana na mavuno yatakayopatikana mkoani hapo.
RC Mahenge akamalizia hotuba yake kwa kuwashukuru wakulima na wadau mbalimbali wa zao la alizeti yakiwemo mashirika na makampuni mbalimbali yaliyojitolea kulima na kuwasaidia wakulima kupata mbegu baada ya ile iliyokuwa inatarajiwa kupitia Wizara ya kilimo kutotosheleza mahitaji.
Mkuu wa mkoa Singida Dkt. Binilith Mahenge akionesha moja ya zao la alizeti wakati alipotembelea mashamba ya wakulima mbalimbali katika Kata ya Mudida Halmashauri ya Singida Vijijini
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskasi Muragili akafafanua kwamba pamoja na kwamba hawakufikia lengo la upatikanaji wa mbegu kama walivyojiwekea malengo, lakini wananchi na mashirika mbalimbali waliweza kuweka jitihada za upatikanaji wa mbegu kwa kununua sehemu mbalimbali jambo ambalo limesaidia kuongeza uzalishaji na kufanya tuvuke malengo alibanisha Mhandisi Muragili.
“Tokea wananchi wa Singida waanze kulima alizeti hawajawahi kulima mashamba makubwa kwa ufanisi kama kipindi hiki, na hii imetokana na uhamasishaji mkubwa uliofanywa na serikali pamoja na ugawaji wa mbegu kwa mkopo. Singida tutavuna alizeti nyingi kuliko miaka yote” Alibainisha DC Muragili.
Mkuu wa Wilaya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akieleza jambo wakati wa ziara hiyo
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Beatus Choaji wakati akitoa taarifa ya kilimo amesema mkoa ulipata mbegu za alizeti tani 469 kwa ajili ya kupanda ekari 239,700 jambo ambalo lilitekelezwa.
Bwana Choaji akaendelea kusema kwamba malengo ya mkoa ilikuwa ni kupata mbegu za alizeti tani 581.9 ambazo zingeweza kuwatosheleza wakulima wote na badala yake wakapata kiasi cha tani 469 ambazo hazikuweza kukidhi mahitaji ya wakulima wote.
Amebainisha kwamba wilaya ya Singida Vijijini imepata mbegu za alizeti tani 76.04 kutoka kwa wakala wa mbegu nchini ASA kupitia Wizara ya kilimo ambazo zimesambazwa katika kata 21 za wilaya hiyo.
Hata hivyo Wilaya hiyo ilipata tani 3.8 za alizeti zilizotolewa na shirika la IFARD ili kuwasaidia wakulima wa zao hilo na kuondoa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kupikia hapa nchini.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Beatus Choaji akitoa taarifa ya kilimo mkoa wa Singida wakati wa ziara hiyo
Akimalizia maelezo yake Bwana Choaji amemuhakikishia Mkuu wa mkoa huo kwamba kutokana na mwitikio mkubwa wa wakulima pamoja na kwamba walipata mbegu pungufu lakini matokeo yatakuwa makubwa na watakuwa wamevuka malengo ya kiasi walichotegemea kuzalisha.
Awali akitoa taarifa ya wilaya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida Nathalia Mosha ameeleza kwamba Halmashauri hiyo ina eneo linalofaa kwa kilimo lipatalo hekta 321,400 ambapo 3, 400 zinafaa kilimo cha umwagiliaji.
Amesema katika msimu wa kilimo wa 2021/2022 wamelima hekta 38,936 na matarajio ni kuvuna tani 73,936 ambapo mbegu za alizeti zilizotumika ni standard seed, Hysun 33, supersun 66 na recod zilizozalishwa na wakulima wenyewe.
Bi. Nathalia Mosha, akitoa taarifa ya kilimo kwa ngazi ya wilaya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida
Mkuu wa mkoa Singida Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo kwa Maafisa Kilimo mkoa dhidi ya wadudu waharibifu
Ziara ikiendelea
Mwisho.
https://www.blogger.com/blog/post/edit/6903235629886141782/3367812376769514275
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.