Mkoa wa Singida umeazimia kuboresha hali ya utoaji na matumizi ya lishe bora katika mkoa huo kwa makundi yote ya watoto na watu wazima ili kuhakikisha wanakua na afya njema itakayowaweka mbali na magonjwa yatokanayo na lishe duni ikiwemo ukondefu, udumavu, upungufu wa damu na uzito pungufu.
Hayo yamejiri katika kikao cha utekelezaji wa hali ya lishe katika ngazi ya Mkoa leo Agosti 22, 2025, kilichowakutanisha Kamati ya Lishe ya Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Halmashauri, Maafisa Elimu, Waweka Hazina, Timu ya RHMT ya Mkoa pamoja na wadau mbalimbali wa lishe.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Victorina Ludovick, alisema kuwa kikao hicho ni sehemu ya jitihada endelevu za kuboresha afya na lishe ya wananchi kwa kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa suluhu za haraka na zenye ufanisi.
“Kwa sasa bado tuna udumavu , ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kwa asilimia 2.3, upungufu wa damu, na uzito pungufu kwa asilimia 11.1. Lakini kikao hiki kinatupa nafasi ya kuweka mikakati mipya ya kupunguza changamoto hizi. Tunapopambana vizuri katika ngazi ya mkoa, mchango wetu kitaifa unakuwa mkubwa zaidi,” alisema Dkt. Ludovick.
Aidha alisisitiza kuwa wataalamu wa afya na lishe, kwa kushirikiana na sekta mtambuka, wanapaswa kuja na mbinu bora zaidi za kupunguza matatizo hayo, ili kuhakikisha Singida inakuwa na wananchi wenye afya bora na taifa lenye nguvu kazi imara.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Mkoa, Bi. Tedda Sinde, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa masuala ya lishe akibainisha kuwa hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo usimamizi shirikishi katika sekta za afya, ustawi wa jamii na lishe, uhakiki wa ubora wa takwimu, utoaji wa elimu ya lishe katika vituo vya afya, jamii, redioni na mashuleni.
“Tumeendelea pia kufanya tathmini ya mara kwa mara ya hali ya lishe na elimu ya magonjwa yasiyoambukiza sambamba na kuhamasisha jamii kulima na kutunza bustani za mboga majumbani. Haya yote yanaimarisha lishe kwa wananchi,” alisema Bi. Sinde.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Bi. Sarah Mkumbo amewasilisha hali ya uvunaji wa chakula mashuleni ambapo ameeleza kuwa kiwango cha upandaji na uvunaji kimepungua mwaka huu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Hata hivyo mashule yetu bado yanapanda mazao ya chakula chenye lishe kwa watoto ikiwemo mahindi, mtama, mpunga, alizeti, karanga, maharage na kunde. Tunapambana kuhakikisha kila mwanafunzi anapata chakula chenye virutubishi,” alisema Bi. Mkumbo.
Mwenyekiti wa kikao hicho Bw.Pancras Stephen akiongoza kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa,Ka yake, ameaziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya lishe zinawasilishwa na kutumika kwa malengo yaliyopangwa.
“Ni lazima tuwe na uwajibikaji mkubwa. Fedha za lishe zisicheleweshwe wala kutumika kinyume na makusudi yake. Vilevile idara mtambuka zinapaswa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za lishe mara kwa mara, huku tukiimarisha ushirikiano na wadau na kuongeza mashine za kuongeza virutubishi kila kata,” amesema Bw. Pancras.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano kuwa kila sekta na kila mtaalamu atashirikiana kikamilifu ili kuimarisha hali ya lishe mkoani Singida. Lengo ni kuhakikisha watoto wanakua na afya bora, watu wazima wanabaki na nguvu kazi imara, na Singida inachangia vyema katika kupunguza changamoto za lishe kitaifa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.