MKOA wa Singida unajivunia kuwa miongoni mwa Mikoa minne (4) nchini, kimkakati katika suala la uzalishaji wa mazao ya kilimo cha alizeti, huku ukipunguza nakisi ya mafuta ya kula na kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya fedha za kigeni ambazo hutumika kuagiza mafuta kutoka nje.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba wakati wa Kongamano la Uzinduzi wa Msimu wa Kilimo kwa mwaka 2023/2024 katika Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Serukamba ambaye amefungua Kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa Mkoa wa Singida unategemea Kilimo na Mifugo kwa asilimia 75 na umekuwa ni kati ya Mikoa ambayo inapambana katika kuhakikisha uzalishaji wa mafuta ya kula yanayotokana na zao la alizeti hapa nchini unaongezeka.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Kitendo cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuufanya Mkoa wa Singida kuwa kati ya Mikoa minne (4) bora ya kimkakati kwa Kilimo ni fursa kubwa kwa wana Singida kuchangamkia fursa hiyo ili kuondokoana na umaskini.
Amesema Mkoa wa Singida katika msimu wa kilimo mwaka 2022/2023 ulizalisha mafuta ya alizeti kwa zaidi ya asilimia 50 ambayo yanatumika hapa nchini pamoja na mazao mengine ambayo yalipatikana Mkoani humo ambapo amewahimiza wakulima kuongeza kasi katika kilimo ili kwa msimu ujao wa 2023/2024 uweze kuongezeka hadi zaidi ya asilimia 80 pamoja na kujitosheleza kwa chakula.
“Mkoa wa Singida katika msimu uliopita 2022/2023 ulifanikiwa kuzalisha vizuri mazao ya chakula na haukuwa miongozi mwa Mikoa ambayo haikujitosheleza kwa chakula katika msimu uliopita”
“Tumefanikiwa kutengeneza ajira zaidi ya vijana na wanawake katika sekta ya kilimo na mazao ya kilimo ambapo ukipita kandokando ya barabara kuu Mkoani Singida utashuhudia akinamama na Vijana wakiuza mafuta ya kula, vitunguu, asali, kukuna mayai” Serukamba akizungumzia mafanikio ya kilimo uchumi na biashara Mkoani Singida
Amesema kuwa kwa Wilaya ya Iramba imenufaika kwa kupata ruzuku ya mbegu ya Alizeti aina ya Record Tani 75 zenye thamani ya sh. Milioni 337.5, pikipiki 34 kwa ajili ya maofisa ugani kwenye Kata zote 20 kwenye Halamashauri ya Wilaya ya Iramba pamoja na Maafisa Ugani 18 ambapo wataalamu wa Mifugo 12 na Kilimo 6 pamoja na wataalamu wa umwagiliaji kutoka tume ya umwagiliaji watatu (3).
“Mheshimiwa Rais ameleta mbolea ya ruzuku ambapo katika msimu uliopita Iramba ilisambaziwa Tani 539 na mwaka huu mpaka sasa wakulima wa Iramba wameshasambaziwa mbolea Tani 475 na kazi ya usambazaji inaendelea.” Serukamba
Katika hatua nyingine Serukamba amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote Mkoani humo kuhakikisha mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Rais Dkt. Samia, wanaisimamia kikamilifu na kuifikisha kwa wakulima wote hadi ngazi ya Kata ndani ya Mkoa huo ili iweze kupatikana kwa urahisi na wakati kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mafuta ya kula nchini na mazao mengine.
Serukamba amesema Mkoa wa Singida kwa miaka yote Sitini (60) toka uhanzishwe haujawahi kufikiliwa kama ungeweza kuwa ni kati ya mikoa minne kinara katika msimu wa kilimo kwa mwaka 2022/23 kutokana na historia ya ukame katika Mkoa.
Serukamba amesema kuwa kongamano hilo limewahusisha wadau kutoka taasisi mbalimbali ndani ya Serikali na nje ya Serikali na kuhudhuriwa na wakulima wapatao 500.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.