Mkuu wa Mkoa wa Singida , Mheshimiwa Halima Dendego, amesema Mkoa wa Singida unazidi kupiga hatua kubwa ya maendeleo,
Amezungumza hayo kwenye Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lililofanyika leo katika ukumbi wa Sekondari ya Mwenge, Mkoani Singida, akisema kuwa Serikali imeweza kuboresha huduma muhimu za jamii, ikiwemo afya, elimu, maji safi, mazingira, na miundombinu ya barabara, hivyo kuchochea maendeleo ya mkoa wa Singida.
Ameeleza, kuwa kutokana na mwendelezo wa miradi inayotekelezwa, wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali, huku akibainisha kuwa miradi mipya inatarajiwa kuanzishwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Shekhe Issah Nassoro, ameyataka madhehebu ya dini, na Taasisi zote za Kiislamu kuimarisha mshikamano, kwa kuwa wanamwabudu Mungu mmoja,chini ya mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW), na kwamba umoja huo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya dini na jamii kwa ujumla.
Shekhe Nassoro amesema kuwa, hakuna taasisi inayopaswa kuleta mgawanyiko miongoni mwa Waislamu kwa sababu yoyote ile, ikiwemo tofauti za kiimani au mapokeo akiwataka viongozi wa madhehebu yote kutumia hekima, busara na mawaidha yenye manufaa kwa jamii badala ya kulaumiana au kuitana majina mabaya kwa sababu ya tofauti ndogo.
Naye Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Singida, Omari Muna, ameipongeza Serikali kwa maendeleo iliyoyaleta, huku akisisitiza umuhimu wa elimu ya mpiga kura, ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao, kwa kupata uelewa wa kutosha akisema uhamasishaji wa wananchi kushiriki katika uchaguzi ni hatua muhimu ya kuhakikisha demokrasia inaimarika na maendeleo ya Taifa yanaendelea kwa kasi zaidi.
Aidha, amepongeza juhudi za madhehebu ya Kiislamu kuweza kuimarisha maendeleo ya kijamii na kutekeleza miradi mbalimbali, akisema hatua hizo zinaendelea kuinua maisha ya waumini na jamii kwa ujumla.
Wito wa kuimarisha mshikamano unakuja wakati ambapo umoja wa kidini unazidi kuwa msingi wa maendeleo, huku waumini wakihimizwa kushikamana na kuepuka migawanyiko ili kudumisha mafanikio ya dini na jamii kwa ujumla.
KARIBU SINGIDA,MEI MOSI 2025..
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.