Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewahimiza wanawake mkoani Singida kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 ili waweze kuwa na nafasi ya kushiriki katika ngazi za maamuzi.
Amesema hayo leo (Oktoba 9,2024) wakati akifungua kongamano la wanawake na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ambalo linawashirikisha wanawake kutoka wilaya zote za mkoa huu lengo likiwa ni kuwahamasisha kujitokeza kushiriki uchaguzi mwaka huu na mwakani huku sambamba na kampeni za uchaguzi zitakazonza rasmi 20 hadi 26 Novemba 2024 huku akiviomba vyama vyote vya siasa vitakavyoweka wagombea kufanya kampeni za kistaarabu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
"Nitumie nafasi hii kuwakumbusha kwamba 27 Novemba, 2024 ni siku ya uchaguzi wa Viongozi wetu wa Serikali za Mitaa (Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji) nchi nzima, Kaulimbiu ya uchaguzi huu inasema “Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo ya Taifa letu, maandalizi yote ya kufanikisha uchaguzi huu yamekamilika kwa kuanza na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura lililofanyika kuanzia tarehe 25 Septemba, 2024 hadi tarehe 01 Oktoba, 2024,"amesema Dendego.
Mheshimiwa Dendego amesema takwimu za wamawake mkoani Singida haziridhishi kwani pamoja na mkoa kuwa na idadi kubwa ya wanawake lakini wenyeviti wanawake ni 96 tu, mitaa ipo 53 wenyeviti Wanawake wapo 03 tu na jumla ya Wanawake katika nafasi ya ujumbe wa Serikali katika ngazi zote wapo 3,125. Aidha, katika nafasi ya Udiwani kati ya Kata 136 za Mkoa, Madiwani Wanawake wapo 04 tu wa kuchaguliwa.
"Takwimu hizi haziridhishi, niwaombe wanawake wenzangu kwa kuanza na uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa twendeni tukapindue meza, tujitokeze kwa wingi kugombea nafasi zote kwani Sifa tunazo, uwezo tunao, vipawa na maarifa ya uongozi tunayo, wanawake ni Jeshi kubwa tukiamua tunaweza," amesema Dendego.
Naye Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa, nchini Anne Makinda,amewataka wanawake katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wajiandikishe,wagombee nafasi za uongozi na kwenda kupiga kura kwa kufanya maajabu katika chaguzi hizo kwa kuhakikisha wanawake wanakuwa wenyeviti wa vitongoji,vijiji na mitaa nao wanakuwa wanawake hadi dunia ishangae.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma R. Mganga, amesema kongamano hili ni kwa ajili ya kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 huku akisema uwakilishi wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi katika mkoa ww Singida ni mdogo sana kwani katika vitongoji 2000 vilivyopo mkoani Singida uwakilishi wa wanawake kwenye uongozi ni asilimia 4 tu huku vijiji 441 vilivyopo Mkoa wa Singida ni wanawake watano tu ndo walipata nafasi ya uongozi kuwa wenyeviti wa vijiji ambao ni sawa na asilimia moja
"Katika Manispaa ya Singida kuna mitaa 53 lakini wanawake waliodhubutu kuchukua fomu na kushinda ni watatu tu wakati katika nafasi ya ujumbe kati ya nafasi 11,000 za wajumbe wa serikali za mitaa wanawake 3,125 ndo wajumbe wa serikali za mitaa," alisema.
Dk.Mganga amehitimisha kwa kusema kuwa kutokana na uwakilishi mdogo wa wanawake katika uongozi serikali ,Mkoa wa Singida hautanyamaza juu ya suala hilo na ndio sababu ya kuandaa kongamano ili kuwapa uelewa na ujasiri wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.