Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga ameiagiza Taasisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kujitangaza kwa kufanya kazi zenye ubora na kutafuta wateja wapya badala ya kutegemea Serikali na Taasisi zake.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 29.03.2023 wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wa TEMESA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo zilizopo Singida mjini ambapo amesema Serikali imetoa mashine na mitambo mbalimbali kwa taasisi hiyo ambazo zinaweza kuwa sababu ya kimbilio kwa wateja wa nje endapo huduma itaboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Mganga ameagiza taasisi hiyo kufanya utafiti na kubaini sababu zinazosababisha upatikanaji hafifu wa wateja huku akibainisha kwamba uboreshaji wa huduma kwa mteja utasaidia kwa kiasi kikubwa Taasisi hiyo kufanya kazi ki biashara.
"Kwa vifaa ambazo Serikali imevileta tunategemea TEMESA iwe kimbilio kwa watu wengi, tangazeni kazi zenu muongeze wateja wa nje ya Serikali na hakikisheni mnaboresha huduma kwa wateja wavutiwe" Dkt. Mganga
Aidha amewataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuondoa malalamiko ambayo yalikuwepo awali yaliyohusu upatikanaji wa vipuri, matengenezo kuchukua muda mrefu na gharama kubwa ya matengenezo ambapo amewataka kuhakikisha wanakabiliana na hali hiyo na kununua vitu kwa pamoja (balk procurement) ili kupunguza gharama kwa wateja.
"TEMESA imeanzishwa ili kutoa unafuu wa utenegenezaji wa magari na umeme pamoja na mitambo kwa bei nafuu kuliko wengine hivyo niwapongeze kama mmeanza hatua za mabadiliko"
Hata hivyo RAS ameishauri Taasisi hiyo kupitia kitengo chake cha usimikaji wa umeme kuandaa mkakati wa kupima umeme katika majengo ya Serikali na Taasisi mbalimbali na kutoa ushauri kwa wamiliki ili kuondoa changamoto za ajali za moto ambazo mara nyingi zimekuwa zikielezwa kuwa zinasababishwa na hitilafu za umeme.
Hata hivyo Dkt. Mganga amesisitiza watumishi hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika kutunza na kutumia mali za Umma na kuwekeza katika matumizi ya TEHAMA katika uhifadhi na ugawaji wa vipuri ili kuepusha upotevu.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Hassani Karonda amesema katika kuboresha huduma zao Serikali katika mwaka wa fedha kwa mwaka uliopita ilitoa milioni 700 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu lakini ambapo kwa mwaka wa fedha ujao wametenga Bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza uboreshaji huo.
Awali akitoa taarifa ya kikao kazi hicho Erasto Cheza fundi mkuu wa Karakana Mkoa wa Singida amesema majukumu ya karakana yao ni kufanya matengenezo ya magari pikipiki na mitambo ya Serikali, utenegenezaji na usimikaji wa mifumo ya Umeme na viyoyozi na ameendelea kueleza kwamba wanatoa ushauri wa kitaalamu nyanja za Mhandisi wa ufundi na umeme.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.