Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari Wilayani Singida wamekabidhiwa vishikwambi 270 kwa ajili ya kufundishia elimu ya afya ya uzazi na kujikinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wanafunzi wa shule 135 za Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Akikabidhi vishikwambi hivyo Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili amesema vishikwambi hivyo vikitumika vizuri vitasaidia kutoa elimu iliyokusudiwa na kufundishia pamoja na kuweka rejea mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya walimu.
Amesema tafiti zimefanyika katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida ikabainika kwamba kuna upungufu wa elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa msingi na sekondari hivyo kuwataka walimu hao kuhakisha kwamba matokeo yanakuwa chanya kwa kipindi kifupi kijacho.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza kabla ya kuwakabidhi walimu vishikwambi hivyo
Amesema kwamba Serikali ina mpango kabambe wa kufanya kazi zake kwa njia ya TEHAMA (E- Government) hivyo utolewaji wa vishikwambi hivyo ni dalili ya Seriakali kuwaandaa watu wake kufanya kazi kwa njia ya mtandao.
Hata hivyo Muragili amewataka walimu hao kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa na kuwafundisha walimu wengine ili kurahisisha kazi hiyo kwa kuwa baadae mashule yatanunua vifaa hivyo kwa ajili ya kufundishia.
Aidha amewashauri walimu hao kupakuwa programu mbalimbali za kufundishia ambazo zipo kwenye mitaala ya shule kwa kuwa kupitia mkongo wa Taifa kumekuwa na vitabu vingi vya kufundishia vinavyopatikana katika mtandao ili kupata mbinu mbalimbali za kufundishia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Singida Vijijini Esther Anania Chaula amesema kupitia mradi wa TASAF chini ya mradi wa Timiza Malengo unajihusisha na elimu ya ujasiriamali pamoja na mitaji kwa wasichana na wanawake wadogo ili waweze kuendesha maisha yao kwa kushirikiana na TAYOA, AMREF na TACAIDS
Amesema mradi huo uliohusika na ugawaji wa vishikwambi unahusisha Halmashauri 20 nchini na Singida DC ikiwa miongoni mwa wanufaika ambapo walitoa elimu kwa walimu 270 ikiwa walimu wawili kutoka shule za msingi 94 na sekondari 41
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Singida Vijijini Esther Anania Chaula akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vishikwambi.
Amesema vishikwambi hivyo tayari vimewekewa program mbili za afya ya uzazi na elimu ya VVU lakini bado zina uwezo wa kuongeza programu nyingine ambazo zinaweza kusaidia katika ufundishaji.
Mkurugenzi huyo akaeleza kwamba vifaa vilivyogawiwa ni vishikwambi, chaja na makasha kwa ajili ya usalama wa kifaa hicho ambapo amebainisha kwamba vitamilikiwa na walimu hao lakini vitakuwa ni mali ya shule husika.
Mwalimu Piusi Chigeso kutoka shule ya Sekondari Maghojoa ameishukuru Serikali kwa kutoa zana hizo kwa ajilia ya ufundishaji na kujifunzia ambapo vitasaidia wanafunzi kuelewa kwa haraka kwakuwa inaonesha kwa vitendo.
Hata hivyo mwalimu Pius akaiomba Serikali kuongeza vitendea kazi hivyo kwa kuwa shule nzima kuwa navyo viwili huenda visilete tija iliyokusudiwa.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.