KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2024, Godfrey Mnzava, amevitaka vyombo vya Watumia maji (CBWSO) kutoa huduma ya maji kwa wananchi wote bila upendeleo na kuendelea kutunza miundombinu ya mradi ili iendelee kutoa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Ametoa agizo hilo leo (Julai 7, 2024) baada ya Mwenge huo kutembelea mradi wa maji uliopo katika kijiji cha Matare Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kujenga miradi ya maji ili kuwawezesha wananchi kuondokana na kero ya ukosefu wa maji hivyo njia pekee ya kuifanya miradi hiyo iwe endelevu ni kutunza vyanzo vya maji.
Aidha, Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ameendelea kusisitiza kuitaka Wakala wa Usambazaji Maji na Safi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) kuziwezesha kimafunzo Jumuiya za Watumia Maji.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ikungi, Shafii Shabani, amesema ujenzi wa mradi huo wa maji ulianza Januari 19, 2022 na umekamilika April 30, 2023.
Amesema chanzo cha maji cha mradi huo ni Kisima kirefu kilichochimbwa katika kijiji cha Matare na chenye kina cha 160m kikiwa na uwezo wa kuzalisha maji lita 5,600 kwa saa na tabgu la kuhifadhia maji linahifadhi lita 75,000.
Shabani amesema mradi huo hadi kukamilika kwake umedharimu 332,736,915.50, ambazo kati ya hizo Sh.327,521,815.50 zimetolewa na Benki ya Dunia kupitia program ya P4R na Sh. 5,215,100 zimetolewa na chombo cha watumia maji (CBWSO).
Meneja huyo ameongeza kuwa faida zamradi huo ni kuwawezesha wananchi wa kijiji cha Matare kupata huduma ya maji safi na salama na ya kutosha kwa matumizi ya kawaida na ya kiuchumi, kupunguza maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama na kuwapatia wananchi muda wa kutosha kufanya shughuli za kiuchumi.
Shabani amesema mradi huu ulisanifiwa kuwahudumia wakazi 5,036 wa kijiji cha Matare lakini kwa sasa mradi unahudumia wakazi 3,083.
MWISHO
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.