Makatibu Tawala Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini, wametakiwa kuwekeza zaidi kwenye vitengo vya mawasiliano serikalini, kwa kuviongezea nguvu za rasilimali na weledi, ili vitekeleze majukumu ya kuihabarisha jamii kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhe Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 23, 2025, wakati akifungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Maafisa Mawasiliano na Habari Serikalini kinachofanyikia jijini Dodoma.
Amesema, Mhe Rais Dkt Samia ameweka historia katika utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo hadi kwenye ngazi za msingi kwa jamii, hivyo ni muhimu kwa taasisi za umma hususani Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuzifikisha taarifa sahihi za mafanikio hayo kwa wananchi, kupitia vyombo vya habari.
Mhe Mchengerwa amesema, hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa zaidi wakati huu ambapo jitihada mbalimbali zinafanyika kupitia taasisi hizo, kukuza na kuendeleza tasnia za habari na mawasiliano kwenye maeneo yao.
Katika kikao hicho, Waziri Mchengerwa alikiri pia kuwepo kwa upungufu wa Maafisa Habari katika baadhi ya maeneo nchini, jambo linaloathiri utoaji wa taarifa kwa umma ambapo amemuagiza Katibu Mkuu kuhakikisha anafanyia kazi suala hilo kwa kuhakikisha kila Mkoa na Halmashauri unapata Maafisa Habari ili kuuhabarisha umma kwa mapana zaidi.
Kadhalika amewataka Maafisa Mawasiliano na Habari Serikalini, kuwa wabunifu na kutambua fursa walizonazo kufikisha taarifa kwa upana zaidi kwenye mifumo ya mawasiliano ya taasisi zao na vyombo vya habari vya umma na binafsi nchini.
”Ninyi ni jeshi kubwa, mpo zaidi ya 200 nchi nzima hivyo mkiamua kutekeleza majukumu yenu ipasavyo, Tanzania na dunia itapata taarifa sahihi kuhusu hatua hizi kubwa za maendeleo yanayofanyika nchini,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe Rosemary Senyamule, ameshauri Maafisa habari kutangaza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika miradi mbalimbali ya kimkakati hata yaliyofikiwa nje ya maeneo yao kama ilivyo treni ya kisasa inayotumia (SGR), viwanja vya ndege ili wananchi wafahamu hata yale yanayofanyika katika Taifa kwa ujumla na sio katika Halmashauri pekee.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, alieleza kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili Maafisa Habari ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi, rasilimali fedha na ushirikiano mdogo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa halmashauri, hali inayorudisha nyuma jitihada za Serikali katika kutoa taarifa kwa wananchi.
Kikao kazi cha Maafisa habari kinalenga kufanya tathimini ya utendaji kazi katika maeneo mbalimbali,kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kadhalika kupokea maelekezo ya Serikali juu ya utoaji wa habari za Serikali na za TAMISEMI.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.