Viongozi na wajumbe kutoka Tume ya Rais ya maboresho ya Kodi wamefika Mkoani Singida kwa lengo la kuzungumza na Wafanyabiashara,wajasiriamali wadogo na wakubwa Mkoani Singida pamoja na kusikiliza kero, changamoto,na kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwao kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa kibiashara na kuongeza wigo wa kulipa kodi.
Wafanyabiashara hao wametoa maoni yao ikiwa ni pamoja na kuiomba Mamlaka ya mapato nchini TRA kuanzisha maduka darasa ili wafanyabiashara wajifunze kupitia maduka darasa hayo kama ambavyo sekta zingine zinafanya,Lakini pia wameshauri ajira za TRA ziwape kipaumbele vijana waliosomea mambo ya kodi ili kuongeza ufanisi katika kusimamia kodi.
Pia wameomba kupunguzwa kwa vizuizi barabarani ambavyo vimekuwa ni changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wanaposafirisha mizigo yao hivyo Tume hiyo iangalie katika eneo hilo na kulitafutia ufumbuzi mbadala.
Aidha,wafanyabiashara hao wameiomba tume hiyo kurejesha vitambulisho vya wafanyabiashara wajasiriamali vilivyokuwa vikilipiwa Shilingi Elfu ishirini ili kuongeza idadi ya walipakodi nchini na kuchochea maendeleo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga akizungumza baada ya kusikiliza kero mbali mbali za Wafanyabiashara amewaagiza TRA kuhakikisha wanafanyia kazi malalamiko yote yaliyotolewa pamoja na kuboresha huduma zao ili ziwe rafiki kwa wateja wao kwa lengo la kuhakikisha ongezeko la mapato katika Mkoa bila kuathiri Wafanyabiashara.
Pia aliwasilisha changamoto ya kukosekana ya uandaaji wa mahesabu ya biashara inayosababisha kufungwa kwa biashara baada ya ukaguzi kwa wafanyabiashara ambao hulalamika kukosekana kwa uwiano wa tozo wanazodaiwa na faida inayopatikana.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Singida akiwapokea wajumbe hao ofisini kwake amesema ni wakati sahihi kwa wao kufika Singida ili kusikiliza maoni na changamoto Wafanyabiashara wanazopitia katika kazi zao.
Amesema kuwa ,makusanyo ya kodi Mkoani Singida yapo vizuri kwani wananchi wanajitambua na wanalipa kodi licha ya changamoto zilizopo ikiwemo elimu ndogo ya ulipaji kodi hususani vijijini,matumizi madogo ya mashine za EFD,na mrundikano wa tozo katika Halmashauri.
Amesema kuwa kama Mkoa wameandaa mikakati ya kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa kushirikiana na TRA pamoja na kusisitiza matumizi ya mashine za EFD kwa wafanyabiashara.Pia kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ikiwemo miundombinu ya barabar na masoko,pia, kutumia rasilimali na vyanzo mbadala kuongeza mapato.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya maboresho ya Kodi,Balozi Ombeni Sefue amewahakikisha wafanyabiashara wa Mkoa wa Singida kuwa wataziwasilisha kero zao zote kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na wataendelea kupokea kero zao kupitia njia mbalimbali ikiwemo barua pepe.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, wakuu wa Sehemu na vitengo, Wakurugenzi wa Halmasahauri, Wakuu wa Taasisi za umma na binafsi, wawakilishi wa Wafanyabiashara, wanawake wajasiriamali na Chama cha watu wenye ulemavu.
@USIKOSE KUFUATILIA MITANDAO YETU YA KIJAMII
INSTAGRAM:SINGIDA RS
FACEBOOK:SINGIDA RS
YOUTUBE:RAS SINGIDA
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.