Maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, leo wameendesha mafunzo kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Watendaji wa Kata wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya rushwa na kuboresha huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo, yamefanyika leo Februari 4, 2025,katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Singida, yamehudhuriwa na viongozi wa Manispaa, ambapo walijikita katika kujua umuhimu wa kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa, hasa kwa namna viongozi wanavyohudumia wananchi. Aidha, walipata pia mada kuhusu uchambuzi wa mfumo wa uondoaji wa taka ngumu ndani ya Manispaa hiyo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa wa TAKUKURU, Bw. Lumemi Kisonga, amewataka viongozi kuwa na uwajibikaji katika maeneo yao kwa kuhakikisha kuwa wanashughulikia malalamiko ya wananchi kwa ufanisi na kwa haki.
Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutambua wajibu wao na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, ili huduma zitolewe bila ubaguzi.
'Viongozi mnatakiwa kuwa mfano wa kuigwa. Hakikisheni kwamba malalamiko ya wananchi yanasikilizwa na kutatuliwa kwa njia zinazofaa huku mkiwajibika katika nafasi zenu. Hii ni sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa," alisema Bw. Kisonga.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TAKUKURU katika kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma na wananchi, na kuhakikisha kuwa mifumo ya utawala inakuwa wazi na yenye uwazi ili kupunguza rushwa katika sekta za umma.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.