Walimu wa somo la Hisabati pamoja na Viongozi wa Elimu ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, wamejengewa uwezo katika kuongeza mbinu mbalimbali za ufundisha wa somo hilo ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hisabati kwa lengo la kuongea ufauli.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mratibu msaidizi, Program ya shule Bora, kutoka Taasisi ya elimu nchini (TET), Mwesiga Kabigumila amesema Wilaya hiyo inanufaika na mafunzo hayo baada ya utafiti na uchanganuzi wa matokeo ya elimu ya msingi mwaka 2022 kuonyesha kiwango cha ufaulu somo la hilo kipo chini ya asilimia 34 ikiwa ni cha chini zaidi kuliko halmashauri zingine sita za mkoa huo.
Kabigumila, alisema mafunzo hayo yanawahusu walimu wa shule za msingi 50 wa somo la hisabati, waratibu kata 10, walimu wakuu 20 na viongozi wengine mbalimbali, wa halmashauri hiyo na mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa Mwesiga, mafunzo hayo yana lengo la kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji bora, hasa kwenye mahiri zenye changamoto darasani, kwa walimu wanaofundisha hisabati ili kuleta mageuzi chanya kwa wanafunzi kufanya vyema zaidi.
“Kufanya vibaya kwa Iramba kwenye elimu ya msingi mwaka 2022, kwa kiwango cha chini sana ya asilimia 34, imekuwa ni moja ya sababu ya kuleta mafunzo haya, ili walimu wapate mbinu, zitakazowasaidia katika ufundishaji wa somo la hisabati,”alifafanua Mwesiga.
Aidha Mwesiga, aliwataka washiriki kuyaelewe mazingira ya wanafunzi wao wanaowafundisha sambamba na kutengeneza zana zinazotoka kwenye maeneo yao rafiki kwa ajili ya kuboresha na kusaidia mbinu za ufundishaji na ujifunzaji somo la hisabati.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu mkoa wa Singida, Sarah Mkumbo, aliwataka washiriki wazingatie mafunzo yanayotolewa na wataalamu wa elimu, ili mbinu wanazopewa ziweze kuleta tija katika somo hilo, na hivyo kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa wilaya ya Iramba.
Mkumbo amesema kuwa, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na uthibiti ubora katika kutekeleza majukumu ya kuwasimamia walimu lakini mafunzo wanayofundishwa yatawajenga kiuwezo na hivyo kuwaongezea maarifa zaidi ya ufundishaji wa kazi zao za kila siku darasani.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.