Waalimu na wahandisi wametakiwa kutumia vizuri rasilimali zinazotolewa na Serikali katika kukamilisha ujenzi wa madarasa mapya na ambayo ujenzi wake unaendelea kwa viwango vilivyo bora ili kuwawezesha wanafunzi kujifunzia katika mazingira mazuri na wezeshi kwa waalimu kufundishia.
Hayo yamezungumzwa leo Mei 26,2025 Mkoani Singida katika Mafunzo ya siku mbili ya waalimu na Wahandisi kujengeana uwezo juu ya ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa katika mradi wa 'Shule Bora' wakijadili juu ya mbinu,taratibu za kutumia kukamilisha ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa vilivyosalia kadhalika na suala la mazingira ya Shule za Msingi.
Akifungua kikao hicho,Mwalimu Winfred Chilumba ambae ni mratibu wa Shule Bora kutoka TAMISEMI amewaasa Waalimu na Wahandisi kuhakikisha wanatumia mafunzo hayo katika kuketa tija kwa thamani ya pesa kuonekana kwa lengo la kuhakikisha shule zote zinakua vizuri kwa majengo mazuri yenye viwango zingativu.
"Katika fedha hizi za serikali tunazopokea tuhakikishe tunaonyesha uthamani wake kwa kumuunga mkono Rais wetu katika utekelezaji"amesema Mwl.Chilumba.
Naye Mratibu wa Program hiyo Mkoani Singida,Bwana Fredrick Ndahani amefafanua kuhusu Shule Bora akisema kuwa Programu hiyo inajikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni ujifunzaji katika kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kuanza na kuhitimu elimu ya msingi,kadhalika katika ufundishaji katika kuwajengea waalimu uwezo wa namna nzuri ya ufundishaji katika madarasa ya awali na ya msingi na pia katika ujumuishi kwa kuhakikisha hakuna mwanafunzi anakosa kabisa haki ya kusoma bila kujali tofauti zao za kimaumbile au jinsia.
Marrystela Emanuel Ndavi, Mwalimu Mkuu Wa Shule ya Msingi Mwembemoja iliyopo Manispaa ya Singida amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuwa na tija kubwa sana kwao kwani wanajifunza mambo mbalimbali yenye manufaa katika kuhakikisha ujenzi bora wa majengo ya shule ikiwemo ujenzi unaozingatia mabadiliko ya tabianchi ikiwemo joto au baridi ili waweze kusoma katika mazingira ya aina zote.
Kadhalika ameainisha sababu za miradi mbalimbali ya ujenzi wa madarasa ya shule kukwama kuwa ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wananchi ambao hushindwa kutoa nguvu kazi pale ambapo kazi huanza ikiwemo uchimbaji msingi,kubeba mawe nakadhalika hivyo kusuasua kwa kazi hiyo.
Programu hii ya elimu Kitaifa inalenga kuboresha ubora,ujumuishwaji na ujifunzaji salama kwa wasichana na wavulana katika Shule za msingi za Serikali nchini Tanzania na inajumuisha jumla ya Mikoa tisa ikiwemo mkoa wa Singida,Dodoma,Katavi,Kigoma,Mara,Rukwa,Simiyu,Pwani na Simiyu ikijumuisha Halmashauri 67,kata 1450,Shule 5,557 waalimu zaidi 49,000 na wanafunzi milioni nne.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.