Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, amewahimiza Viongozi wa Serikali na wa Dini katika ngazi zote kuanza kampeni ya kuhamasisha wazazi kuwapeleka wasichana wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14 kwenda kupata chanjo ya mlango wa kizazi ili kuwaepusha kupata saratani hiyo ambayo imekuwa ikileta madhara makubwa katika kundi hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida ametoa kauli hiyo kwenye kikao kilichojumuisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Dini, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Wataalamu wa Afya kutoka Wilaya zote za Mkoa huo.
Halima Dendego amesisitiza Wataalamu wa Afya Mkoani Singida kujipanga ipasavyo na kuweka mipango mizuri itakayosaidia wasichana lengwa wanapata chanjo hiyo bila kukosa Mijini na Vijijini.
Naye, Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Singida, Jadili Mhanginoma, amesema Serikali Mkoani Singida inatarajia kutoa chanjo hiyo kwa wasichana 178,114 wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 kuanzia Aprili 22 hadi 26 na kuendelea hadi Desemba mwaka huu.
Ameeleza kuwa kwa sasa tayari dozi 191,040 zimeshapokelewa na kusambazwa kwenye ngazi za Halmashauri mkoani Singida.
Mratibu huyo wa Chanjo amesema chanjo ya Mlango wa Kizazi - HPV- inafaida kubwa ikiwemo kutoa kinga kwa wasichana kutopata virusi vya saratani mbalimbali ikiwemo ya mlango wa kizazi.
Kwa Tanzania chanjo ya Mlango wa Kizazi - HPV- iliidhinishwa kuanza kutumika na Shirika la Afya Duniani kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba – TMDA – mwaka 2014 ambapo kwa mkoa wa Singida chanjo hiyo ilianza kutumika mwaka 2018.
Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Singida, Jadili Mhanginoma, akitoa taarifa ya utoaji wa Chanjo ys HPV ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa Wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kwenye kikao cha uhabarisho ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.