Watumishi watakao bainika kufanya manunuzi bila kuwa na risiti au kufanya malipo hewa kinyume na utaratibu wa Sheria wanatakiwa kulipa madeni hayo kupitia mishahara yao ili kuepukana na tabia ya kuzalisha madeni yasiyotarajiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge alipokuwa akihutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo likiwa linapita hoja za ukaguzi wa hesabu za Serikali.
RC Mahenge amesema kwamba kila Mkuu wa Idara anatakiwa kuwa na risiti kulingana na manunuzi yaliyofanyika katika eneo lake ili kuepusha hoja za ukaguzi na endapo kiongozi hataweza kutekeleza hilo atalazimika kukatwa fedha hizo kwenye mshahara wake.
"Ni lazima tunapofanya manunuzi ya kitu chochote tuwe na risiti na kwa zile hoja ambazo zimebaki tuhakikishe tunatafuta risiti kwakuwa hoja za ukaguzi hazimalizwi kwa maneno" alieleza RC Mahenge .
Aidha RC Mahenge ameagiza Watumishi wa Halmashauri zote Mkoani hapo kuwa na taarifa ya fedha zote zilizotumika kwenye miradi na kuzisambaza kwa Madiwani ili wajue fedha zilizotumika katika Kata zao na iwe rahisi kufuatilia kama kuna madeni ndani yake au vinginevyo.
Aidha Dk. Mahenge amepongeza Baraza hilo kwa kuwa na ufuatiliaji mzuri wa makusanyo jambo ambalo lilisababisha Wilaya hiyo kupata asilimia zaidi ya sabini katika kipindi kilichopita.
Hata hivyo amewataka viongozi hao kuendelea na mshikamano walio nao kwa kuwa utawaletea mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa miradi mbalimbali inayoendelea Wilayani hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo Juni 14, 2022
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, DC Sophia Kizigo alisema mafanikio wanayoyapata yakiwemo kufikia asilimia 95 ya makusanyo waliyopangiwa yametokana na utendaji kazi mzuri wa Madiwani wote wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
DC Kizigo akatumia muda huo kutoa angalizo kwa Wananchi wa Mkalama ambao wanaendelea kufanya Biashara ya mazao kuhakikisha wanabakisha akiba ya chakula itakayowafikisha mwaka ujao.
Amesema Wilaya pamoja na kuwepo kwa mvua za chini ya kiwango katika baadhi ya maeneo huku maeneo mengine ikiwa juu ya kiwango kulisababisha wakulima wengi kupata mazao mbalimbali ya kutosha hivyo kuwataka wananchi hao kuuza kiasi na kubakiza akiba ya chakula.
"Mkalama tuna chakula cha kutosha lakini wasiwasi wetu ni kwa majirani ambao huenda hawakupata mazao katika msimu huu hivyo wakulima wetu hutumia fursa hiyo kuuza mazao yao, jambo ambalo kama hatutakuwa waangalifu litatugharimu" alifafanua DC Kizigo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Asia Messos amesema Kamati ya Bunge walitoa kuhusu hoja mbalimbali ambapo maelekezo yote yamekwishafanyiwa kazi.
Aidha amesema Halmashauri imejiwekea mkakati mbalimbali ikiwemo kuonesha kitengo cha utunzaji wa nyaraka, kuimarisha usimamizi wa fedha kwa kufuata Sheria na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani kuhakikisha hoja za ukaguzi hazitokei.
Mikakati mingine ni kuchukua hatua stahiki kwa Watumishi watakaosababisha kutokea kwa hoja za ukaguzi kwa uzembe, kuomba kuongezewa Watumishi hasa Idara ya fedha na kitengo cha manunuzi na kuongeza matumizi ya mashine za kielektroniki. Aliendelea kufafanua Mkurugezi Asia.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo Bosco Samweli amemuahidi Mkuu wa Mkoa kwamba Madiwani wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wanawaletea maendeleo Wananchi na kwamba hoja za ukaguzi hazitokei katika Halmashauri zao.
Amesema kwa upande wa makusanyo Baraza limejipanga kuhakikisha wanafikia asilimia mia moja au zaidi kulingana na mikakati na ushirikiano wao na Serikali na Wananchi.
Mkutano ukiendelea
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.