Watumishi wa serikali Mkoani Singida wametakiwa kutumia weledi wao katika kutekeleza majukumu ya kila siku ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri masaa ya kazi na yale ya ziada kwa kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi ili kuwaletea maendeleo yaliyokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika leo katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambapo alisistiza wafanyakazi kujua na kutekeleza wajibu kwa umahiri zaidi.
RAS huyo akaendela kusema kwamba, inapotokea mtumishi amepata mafunzo ndani au nje ya nchi, ya muda mrefu au mfupi anapaswa kuonesha ujuzi aliokuwa nao kwa kufanya kazi kwa umahiri ambapo anatakiwa kuwa tofauti na wakati akiwa hajapata mafunzo hayo.
Lengo la serikali la kumuongezea mtumishi maarifa ni kumfanya awe na utendaji wa tofauti na awali na akawe mtumishi mwenye Tija, na ikatokea mtumishi hatimizi takwa hilo atakuwa anaitia hasara serikali. alilisistiza Mwaluko.
Aidha RAS huyo akaendelea kufafanua juu ya zoezi la uchaguzi wa wafanyakazi hodari ambao unatarajiwa kufanyika hivi karibuni na kuwataka wajumbe wa chama cha wafanyakazi TUGHE kuhakikisha vigezo vya kumpata mfanyakazi bora vinazingatiwa ili uhodari huo uweze kuonekana.
Dorthy ametoa wito kwa wajumbe wa baraza hilo na watumishi wa Mkoa wa Singida kuchagua mtu kwa utendaji bora wa majukumu yake na isiwe ni kumchagua kwa kuangalia sura au kuchaguana kwa zamu.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Bw. Deogratius Yinza akijibu hoja za wajumbe kuhusu kuongeza idadi ya watumishi na mpango wa mafunzo kwa mwaka 2022/23 amesema Serikali ina mpango wa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali na kubadilisha vyeo vya baadhi ya watumishi ili kuongeza tija.
Bwana Yinza akaendelea kubainisha kwamba tayari Mkoa umekwishaanda mpango wa mafunzo kwa watumishi ambao ndio utakaotumika kutambua aina ya watumishi na aina ya shule ambazo mtumishi atakwenda .
Awali akiwapitisha wajumbe wa mkutano huo Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Singida Bi Beatrice Mwinuka amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/23 mkoa umejiwekea vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuongeza makusanyo ya mapato kwa kuimarisha usimamizi na udhibiti ili kuondoa mianya yote ya upotevu wa mapato.
Bi. Mwinuka amesema mkoa umedhamiria kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji ili Halmashauri ziwawezeshe wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya wanawake na vijana.
Hata hivyo Mwinuka akaendelea kufafanua kwamba mwaka wa fedha 2022/23 mkoa wa singida umeendelea kujipanga kuboresha mazingira ya uwekezaji viwanda vikubwa na vidogo kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha amebainisha kwamba mikakati hiyo inahusisha kuongeza kiwango cha taaluma katika shule za Msingi na sekondari kwa kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa karibu kama sehemu ya kuleta mabadiliko makubwa ya elimu.
Akimalizia wasilisho lake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mipango na uratibu akaongezea kwamba kwamba sekretarieti ya Mkoa wa Singida katika kipindi cha mwaka 2022/23 imetenga jumla ya Tsh.Bilion 7.6 zitakazotumika katika matumizi mbalimbali ya mkoa.
Akifafanua kiasi hicho cha fedha Beatrice ameeleza kwamba katika Tsh.Bilion 7.6 zilizotengwa kiasi cha Tsh. Billion 5.02 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Tsh.2.78 ni mishahara kwa ajili ya wafanyakazi wakati Tsh. Billion 2.23 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Akizungumzia uendelezaji wa miradi ya maendeleo Bitrice akaendelea kueleza kwamba mkoa umetenga Tsh.Bilioni 2.62 kwa ajili ya miradi hiyo huku akibainisha kwamba kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 443.73 ni fedha za nje wakati fedha za ndani zikiwa Bilioni 2.184.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha wafanyakazi TUGHE Mkoa wa Singida Ethel Kahuluda akaipongeza sekretarieti ya Mkoa huo kwa kuweka stahili mbalimbali za wafanyakazi katika bajeti zao na kuwasihi kwamba zitumike kama zilivyopangwa
Katibu huyo akiendelea na pongezi hizo akamkumbusha muajiri kuhakikisha kwamba watumishi wanapata mafunzo stahiki ili kuboresha utendaji kazi wao huku akiwakumbusha watumishi kuyatumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko chanya katika kazi zao.
Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa sekretarieti ya Mkoa wa Singida, Mtaalamu kutoka Sekretarieti ya Maadili, Makatibu Tawala wa wilaya za Manyoni Iramba, Singida vijijini, Manispaa ya Singida, ,Tughe, Wajumbe na Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Tughe.
Picha ya pamoja
Mwisho.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.