Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeibuka mshindi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 kwa Kanda ya Tatu, na kukabidhiwa kikombe na fedha sh. milioni moja, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Halima Dendego.
Ikungi imeshinda kwenye Kanda ya Tatu yenye mikoa ya Ruvuma, Singida, Dodoma, Manyara, Kagera na Mara, ikiwa ni ishara kuwa walikidhi vigezo kuanzia mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, hamasa, na ubora wa miradi ikiwemo miradi kuakisi thamani ya fedha, na kuwepo kwa vielelezo vyote vya manunuzi na vifaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi, alisema ushindi huo ni wa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wote wa Singida, na imewapata moyo kuweza kuendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa miradi.
Kijazi amesema wao kama viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu, fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, wananchi na wafadhili, watahakikisha inakamilika na kuwanufaisha wananchi.
Mwenge wa Uhuru 2024 katika Wilaya ya Ikungi umezindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi saba yenye thamani ya sh. 3,046,807,381. Na miradi hiyo ipo kwenye sekta ya elimu, maji, afya, mazingira, barabara, ujenzi na maendeleo ya jamii.
"Chanzo cha fedha za miradi hiyo, Serikali Kuu sh.2,889,821,381, wananchi sh. milioni 120, wahisani sh 24,486,000, na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi sh. milioni 12.5" amesema Kijazi.
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava amesema moja ya changamoto kwenye halmashauri hapa nchini ni kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kwa kutumia fedha za mapato ya ndani. Lakini pia, miradi inayotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kushindwa kukidhi haja ya wananchi, hivyo kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, maeneo hayo mawili yapewe kipaumbele kwenye kuangaliwa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.