Mkoa wa Singida leo umeadhimisha Siku ya Vijana Duniani katika hafla iliyofanyika Wilaya ya Ikungi, ambapo vijana wametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa vijana wa Mkoa wa Singida Ndg.Fredrick Ndahani amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya vijana kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mikopo ya Asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia Halmashauri,Programu za mafunzo ya stadi za maisha kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,Mafunzo ya kilimo cha kisasa na ufugaji kupitia mpango wa BBT kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kwa upande wa Mkoa wa Singida, Ndahani amesema katika mwaka wa fedha uliopita, jumla ya Shilingi 1,361,894,654.66 zimetolewa kwa vikundi 147 vya vijana kutoka Halmashauri zote za mkoa huo. Aidha, katika sekta ya elimu, Serikali imetoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari, mikopo ya elimu ya juu, na ufadhili wa "Samia Scholarship".
Ameongeza kuwa Serikali imetumia Shilingi Bilioni 41.9 kujenga madarasa 422, vyoo 905, mabweni 28 na maabara 43, pamoja na ujenzi wa shule za amali katika kila wilaya na shule moja ya amali ya mkoa.
Katika wito wake, Ndahani amewataka vijana kutumia ipasavyo mikopo na fursa zilizopo, kuimarisha mshikamano wa vikundi, kushirikiana na viongozi wa serikali na wadau, kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, na kwa wanafunzi, kusoma kwa bidii.
Amehitimisha kwa kuwasihi wazazi na jamii kuendelea kuwalea na kuwaunga mkono vijana, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano wa taifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu "Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu", ikisisitiza umuhimu wa vijana kama rasilimali muhimu ya taifa katika kuchochea maendeleo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.