Viongozi wa elimu na wadau mkoani Singida wametoa wito wa mshikamano na ushirikiano katika kusimamia fedha na miradi ya elimu ili kuhakikisha ubora wa shule na mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote sambamba na kuhakikisha watoto wote wanapelekwa shuleni kupata elimu bila kuwaacha nyuma wale wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu wa viungo ili kuhakikisha makundi yote yanapata elimu iliyo bora.
Hayo yamejiri katika kikao cha tathimini ya mradi wa Shule bora kwa mwaka 2024/25 Mkoani Singida katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida leo Agosti 14,2025 ambacho kimehusisha Wakurugenzi wa Halmashauri,Wadhibiti ubora wa Shule,Maafisa elimu,wahasibu na Maafisa mipango kutoka Halmashauri za Mkoa wa Singida.
Akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa programu ya Shule Bora, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Bi.Anastazia Tutuba amewataka wakurugenzi wenzake kushirikiana na wataalamu wa elimu, wahasibu, na wadhibiti ubora ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinapangiwa mpango kazi wenye vipaumbele na kutekelezwa kwa wakati. Amesisitiza kuwa kila mtoto ana haki ya kupata elimu bora katika mazingira salama, na kwamba mpango wa Shule Bora hauwezi kubagua jinsia wala changamoto za kimaumbile.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida Dkt.Elpidius Baganda ametoa wito kwa wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kuhakikisha wanawapeleka shule ili wapate haki yao ya msingi ya elimu. Amesema kuwa kuwatenga au kuwafungia ndani watoto hao ni kosa la jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka. Amesisitiza pia kuwa shule zimeboreshwa ili kuwa rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu kwa kujengwa madarasa yanayokidhi mahitaji yao.
Aidha, alieleza kuwa vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu chini ya utekelezaji wa Shule Bora ni pamoja na kuimarisha uandikishaji wa wanafunzi, kuongeza idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi, kuimarisha ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoingia sekondari, kuimarisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kusaidia serikali kufikia vigezo vya EPforR II ili kupata fedha za motisha kutoka kwa wahisani wa maendeleo.
Awali akiwasilisha mada katika kikao hicho,mratibu wa Shule Bora Mkoa wa Singida Bw. Fredrick Ndahani amewasilisha baadhi ya matokeo ya muda mfupi yaliyokusudiwa na mradi wa Shule Bora ikiwa ni pamoja na wazazi na jamii kushiriki kikamilifu katika kuboresha ujifunzaji, walimu kusaidiwa kufundisha elimu bora, jumuishi na katika mazingira salama, shule kusimamiwa kwa uwajibikaji kwa wadau, tawala za mikoa na mitaa kusimamia shule vizuri, pamoja na taasisi za kitaifa kusimamia utoaji wa elimu bora kwa ufanisi.
Bw. Ndahani alihitimisha kwa kusisitiza kuwa utekelezaji wa Shule Bora mkoani Singida unaendelea kuleta mabadiliko chanya katika elimu, huku akiwataka wadau wote kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Nae Mdau wa elimu, Bi. Zipora Semwanza, amesema matarajio baada ya kikao hicho ni kufanya maboresho pale ambapo hapakuwa na ufanisi na kuimarisha maeneo yanayoendelea vizuri huku akiahidi kuwa kutakuwa na maboresho ya miundombinu ya elimu, kuimarishwa kwa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), pamoja na mafunzo kwa walimu ili kuongeza ujuzi, ubunifu na mshikamano wa kiutendaji.
Shule Bora ni programu ya kitaifa inayolenga kuboresha ubora wa elimu, ushirikishwaji, na kuhakikisha mazingira salama ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa shule za msingi za serikali nchini Tanzania. Programu hii inafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kwa idhini ya Serikali ya Uingereza na inatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na mashirika ya Cambridge Education, ADD International, International Rescue Committee (IRC) na Plan International.Kadhalika mradi huo pia unaunga mkono utekelezaji wa mpango wa Elimu wa Kitaifa wa Lipa Kulingana na Matokeo (EPforR II).
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.