Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi leo tarehe 27 Januari, 2025, ikiongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, imezindua kampeni ya upandaji miti chini ya kauli mbiu isemayo “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti,”
ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Zoezi hilo la upandaji miti limefanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi na Shule mpya ya Msingi Mshikamano, ambapo watumishi wa Halmashauri, walimu pamoja na wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari za Unyahati walishiriki kikamilifu, na zaidi ya miti 200 ilipandwa.

Akizungumza katika tukio hilo, Dkt. Mganga alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri wa kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa msimu wa mwaka 2025/2026, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi inatarajia kupanda jumla ya miti 1,500,000 ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda, kivuli na mbao, kwa kushirikiana na wadau wa mazingira waliopo wilayani.

Hadi sasa, Halmashauri imefanikiwa kusambaza miche ya miti 3,200 katika maeneo mbalimbali ya wilaya, ikiwemo Shule ya Msingi Puma na Kijiji cha Mnangana kilichopo katika Tarafa ya Sepuka.

Baada ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti, Dkt. Mganga aliendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo leo tarehe 27 Januari, 2026, katika kata za Misughaa, Puma na Unyahati, kwa lengo la kujiridhisha na maendeleo ya utekelezaji wa miradi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Katika Kata ya Misughaa, alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya kinachogharimu Shilingi milioni 250, ambacho kipo katika hatua ya upauaji, na kinatarajiwa kukamilika mwezi Februari.
Katika Kata ya Puma, alitembelea Shule ya Msingi Puma B inayogharimu Shilingi milioni 545.4, ambapo aliagiza kuongezwa kwa idadi ya mafundi ili kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya tarehe 15 Februari 2026.

Ziara hiyo ilihitimishwa katika Shule ya Mshikamano iliyopo Kata ya Unyahati, mradi unaogharimu takribani Shilingi milioni 302.2, unaotekelezwa kupitia Mpango wa BOOST kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, na upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Akihitimisha ziara hiyo, Dkt. Fatuma Mganga amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli lazima yaende sambamba na utunzaji wa mazingira, akibainisha kuwa miradi ya elimu na afya haina maana ikiwa mazingira hayalindwi kwa ajili ya kizazi kijacho.

Ameagiza wasimamizi wa miradi kusimamia kikamilifu ubora na muda wa utekelezaji, huku akiwaelekeza viongozi na wananchi kushiriki kwa dhati katika utunzaji wa miti iliyopandwa na matumizi ya huduma za kijamii, ikiwemo Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha Ikungi inapata maendeleo endelevu na salama.





SINGIDA
Postal Address: P O BOX 5 SINGIDA
Telephone: 2502170, 2502089
Mobile: 2502170, 2502089
Email: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.