Katika hatua muhimu ya kuhakikisha uzalishaji wa Alizeti unaongezeka, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Bi. Upendo Naftali, ameongoza kikao cha kupanga mikakati ya usambazaji wa mbegu za alizeti aina ya Sunbloom, ambapo halmashauri hiyo imepokea jumla ya tani 12 za mbegu kutoka kwa Wakala wa Mbegu za Serikali (ASA).
Kikao hicho kilifanyika Februari 6, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi za Manispaa ya Singida, na kuhudhuriwa na Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo, Maafisa Elimu Kata, pamoja na Watendaji Kata.
Lengo kuu la kikao hicho ni kuhakikisha kuwa mbegu za alizeti zinawafikia wakulima katika kata zote 18 za manispaa, ili kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima wa alizeti.
Bi. Upendo Naftali alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa kata na maafisa ugani ili kufanikisha malengo ya kuongeza uzalishaji wa alizeti. Aidha, alieleza kuwa usambazaji wa mbegu hizo unafanyika kwa haraka ili kutoa fursa kwa wakulima kupanda mbegu hizi kwa wakati na kuvuna mavuno bora.
Kikao hiki kimejikita katika kuhakikisha kwamba usambazaji wa mbegu unakuwa na mpangilio mzuri ili kuepuka changamoto zozote zinazoweza kuzuia wakulima kufaidika na fursa hii muhimu ya kilimo cha alizeti.
Wakulima wa alizeti katika manispaa ya Singida wanatarajiwa kupata mbegu bora ambazo zitawawezesha kuongeza tija katika kilimo hicho, na hivyo kuchangia katika maendeleo ya kilimo cha mazao ya kibiashara katika mkoa wa Singida.
SINGIDA
Postal Address: P O BOX 5 SINGIDA
Telephone: 2502170, 2502089
Mobile: 2502170, 2502089
Email: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.