Jeshi la Polisi Mkoani Singida, limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kutoka ajali 69 kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi kufikia ajali 24 katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Juni mwaka huu.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ACP Debora Magilingimba wakati akitoa taarifa ya uhalifu kwa Mkoa wa Singida ambapo amesema katika ajali hizo 24 zilisababisha vifo vya watu 29 na hapajakuwepo majeruhi kabisa.
ACP Magiligimba amesema kupungua kwa ajali kumetokana na Jeshi hilo kutoa elimu ya usalama barabarani mara kwa mara hasa katika maeneo ya vijijini, mitaani na hata katika mafunzo ya udereva.
Ameongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likithibiti mwendo kasi katika barabara kuu, kuthibiti ulevi kwa upimaji wa kilevi kwa madereva wote wa vyombo vya usafiri na hivyo kupelekea ajali kupungua sana kwa Mkoa wa Singida.
“Pia tumeendelea kutoa elimu ya usalama barabarani mashuleni, vyuoni na katika nyumba za ibada. Lengo ni kuiongozea jamii uelewa zaidi unaohusu masuala yote ya ulinzi na usalama, na sheria za usalama barabarani”, amefafanua.
Aidha, ACP Magiligimba amesema makosa madogo yamepungua kwa asilimia 0.8 ambapo jumla ya makosa madogo 22,222 yameripotiwa katika kipindi cha januari hadi juni mwaka huu, ikilinganishwa na makosa kama hayo 22,403 yaliyotokea kipindi kama hicho mwaka jana.
“Katika makosa hayo madogo, jumla ya wakosaji 21,836 walilipa faini mbalimbali zaidi ya shilingi milioni 655. Katika kipindi kama hicho mwaka jana jumla ya wakosaji 21,778 walilipa faini mbalimbali zaidi ya shilingi milioni 653.3. Faini hizo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.3”, amesema kamanda huyo.
ACP Magiligimba ametaja baadhi ya mikakati mbalimbali ya kukabiliana/kupunguza zaidi uhalifu, wahalifu na ajali za barabarani kuwa ni kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia vyombo vya habari na kushirikiana na asasi mbalimbali katika kutoa elimu na matengenezo ya barabara.
“Vile vile tutaendelea kuimarisha ushirikiano zaidi na asasi zisizo za kiserikali, ikiwemo World Future Vocation, mabalozi wa usalama barabarani na SUMATRA. Pia tutashirikiana na TANROADS, halmashauri za wilaya na manispaa kushauriana namna ya kufanya matengenezo ya barabara katika maeneo yaliyoharibiwa au yenye kusababisha ajali za mara kwa mara”, amesema ACP Magiligimba.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.