Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewatoa hofu wakulima wa dengu katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwamba tani 257,933 ambazo bado hazijauzwa kwamba zitauzwa na watalipwa fedha zao.
Akizungumza hayo leo Novemba 10,2024 baada ya kutembelea ghala la kuhifadhia dengu lililopo Itigi mjini, amesema serikali itahakikisha dengu iliyopo inauzwa na kwamba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi hadi sasa zimeuzwa zaidi ya tani 15 000.
"Dengu yetu kutoka Mkoa wa Singida tunauza nchini India,bahati nzuri hadi sasa sijapata malalamiko yeyote ya kwamba labda dengu yetu haina ubora hili jambo la kujivunia,"amesema.
Dendego amesema changamoto ambazo zimepatikana wakati wa utekelezaji wa ununuzi wa dengu kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani zitaendelea kutatuliwa na kwamba hivi karibuni kutaitishwa kikao cha wadau kujadili namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
"Zipo changamoto za ukosefu wa maghala,vyama vya ushirika kufa,mizani na AMCOS kupitia kikao ambacho wadau ambacho tutakifanya changamoto hizi tutazojadili na kuona namna ya kuzipatia ufumbuzi,"alisema.
Awali Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Mlagazi Mgalula, amesema zao la dengu limekuwa la kwanza kwa kuingiza mapato kwenye halmashauri ambapo tangu ununuzi ulipoanza Agosti Mosi, 2024 kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani wakulima wameweza kulipwa zaidi ya Sh.bilioni 19.
Amesema hivi sasa kuna changamoto ya upatikanaji wa wanunuzi katika dengu iliyopo kwenye ghala na kwamba halmashauri imefanya mipango kutafuta wanunuzi wengine badala ya kutegemea kuuza India tu.
Katibu wa AMCOS ya Mlowa, Emmanuel Daniel, amesema hivi sasa kuna wiki tatu bado minada haijafanyika hali ambayo imezua hofu kwa wakulima hasa ikizingatia kipindi hiki ni cha kuelekea msimu wa kilimo.
Daniel ameiomba serikali kufanya haraka kutafuta wanunuzi katika dengu iliyopo kwenye ghala ili wakulima waweze kulipwa fedha zao na hivyo wapate nguvu kuandaa mashamba yao.
Issa Adam Issa,mkulima anayefaidika na mfumo wa stakabadhi ghalani,ameonyesha kufurahishwa na mfumo huo amesema umekuja kuwanufaisha wakulima na kuhakikisha wanauza mazao yao kwa bei nzuri,ametoa wito kwa serikali kuhakikisha wanaboresha zaidi huduma hiyo ili watu wengi zaidi waweze kujiunga kwa kutumia njia mbalimbali kuwaelimisha hasa kwa kutoa elimu zaidi juu ya mfumo wa stakabadhi ghalani.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.