Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amezindua mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajasiriamali kuhusu matumizi ya GS1 Barcodes na QR Codes, akisisitiza kuwa mifumo hiyo ya kidijitali ndiyo njia ya kuwafungulia wajasiriamali milango ya masoko ya kitaifa na kimataifa. Mafunzo hayo yamefanyika chini ya kauli mbiu “GS1 Barcodes: Kiungo chako kwa wauzaji rasmi”, yakilenga kuwajengea wajasiriamali uelewa wa mifumo ya utambulisho wa bidhaa inayotambulika duniani kote.

Semina hiyo imewezeshwa na GS1 Tanzania kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo TRA, BRELA na wadau wengine, ambao wameeleza kwa kina namna wajasiriamali wanaweza kupata barcode na QR code kisheria, hatua zinazowaepusha na ulaghai na kuwalinda dhidi ya matumizi mabaya ya bidhaa zao na makampuni mengine. Aidha, hatua hii ya kidijitali inatarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa za Singida na kuziwezesha kupenya kwenye masoko makubwa duniani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Dendego amewataka wajasiriamali wa Singida kuchangamkia fursa hii ya kimkakati, akibainisha kuwa Mkoa wa Singida una bidhaa nyingi zenye ubora wa juu lakini bado hazijapata nafasi ya kutamba kimataifa kutokana na kukosa utambulisho wa kidijitali. “Kundi hili la wajasiriamali ni injini ya uchumi wa Singida. Sisi tuna bidhaa nzuri sana, lakini bila mifumo ya kimataifa kama barcode hatutaifika dunia. Soko la kimataifa linaendeshwa kidijitali, na kama hatuko huko, basi hatutapenya,” amesema.

Ameongeza kuwa Singida ni kitovu cha nchi na hivyo ni mahali sahihi kufunguliwa kwa ofisi ya pili ya GS1 Tanzania. “Ikiwa mtapanga kufungua ofisi mpya nchini, basi Singida ndiyo mahali pake. Tupo katikati ya Tanzania, wajasiriamali watapata huduma kwa urahisi, na hilo litakuwa chachu ya maendeleo makubwa,” amesema.

Mkuu wa Mkoa pia amesisitiza umuhimu wa kulinda amani ili biashara ziendelee kustawi. “Amani ikitoweka, biashara hazipo. Tunaishukuru serikali kwa kutengeneza mazingira bora ya biashara huru. Basi nasi tuitumie fursa hii kutangaza Singida duniani,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Rasilimali Watu, Bw. Pancras Stephen, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi, hasa kutokana na ukweli kwamba hata watumishi wa umma wengi wanajihusisha na ujasiriamali. Amesema, “Ujasiriamali wa sasa uko kwenye mifumo ya kidijitali. Tunawaomba mjenge uthubutu na kutumia maarifa haya kupiga hatua katika familia, jamii na taifa.”

Aidha Katibu Tawala Msaidizi – Biashara na Uwekezaji, Bi. Donatira Vedasto, amewataka wajasiriamali kuwa mabalozi wa Singida kupitia bidhaa zao. “Baada ya mafunzo, kila mmoja achukue hatua. Singida inazalisha bidhaa bora sana, lakini bila barcode hatuwezi kufika soko la kimataifa,” amesema.

GS1 Tanzania, kupitia wakufunzi wake, wameahidi kuendelea kutoa mafunzo katika wilaya zote za Singida. Wamesema wajasiriamali wengi wamekuwa wakikosa nafasi ya kuuza kimataifa kwa sababu hawana elimu ya barcode. “Mafunzo haya yatafanya kila mjasiriamali awe na hamu ya kufika soko la kimataifa. Tutafika kila halmashauri kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,”.

Nao Wajasiriamali walioshiriki semina hiyo wametoa shuhuda wakisema matumizi ya barcode yamewasaidia kuaminika katika supermarkets na malls, hatua iliyoimarisha mauzo na kuwapa nafasi ya kutambulika rasmi na serikali. Wameshukuru serikali kwa kuweka miundombinu ya kidijitali na kuwawezesha kufikia masoko makubwa nje ya nchi.

Hatua hii ya kidijitali imeelezwa kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa ya biashara Singida, huku serikali na wadau wakiahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa ukuaji wa uchumi wa wajasiriamali.




SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.