Wananchi Mkoani Singida,wamepongeza uzinduzi wa Kliniki ya Huduma za Msaada wa Kisheria uliofanyika Singida, wakisema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa haki, kupunguza gharama za kufuata huduma za kisheria na kuongeza uelewa wa masuala ya sheria, haki za binadamu na utawala bora kwa jamii.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi walisema kliniki hiyo imewapa fursa ya kupata msaada wa kisheria karibu na walipo, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishindwa kufikia huduma hizo kutokana na umbali na gharama. Walisema huduma hiyo itasaidia kutatua migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi na masuala mengine ya kisheria yanayowakabili.
Katika uzinduzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Dk. Juma Homera, alisema Wizara ina mpango wa kuandaa sera ya kitaifa ya msaada wa kisheria itakayoweka misingi ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma hiyo nchini, hatua itakayoongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi wengi zaidi.
Dkt. Homera alisema maeneo yatakayoboreshwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya Tehama katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi na kwa wakati.

Alisema utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria umeleta mafanikio makubwa, ambapo tangu kuanza kwake wananchi 3,734,157 wamepatiwa elimu kuhusu masuala ya kisheria, haki za binadamu na utawala bora, jambo alilosema linaonesha umuhimu wa kuendelea na huduma hiyo kwa mwendelezo endelevu.

“Huduma ya msaada wa kisheria imekuwa endelevu na itaendelea kutolewa katika halmashauri zote. Serikali itaendelea kuimarisha huduma hizi ili wananchi wajitokeze na changamoto zao zipate ufumbuzi,” alisema Dk. Homera.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuanzisha na kuimarisha madawati ya msaada wa kisheria katika ngazi ya halmashauri zote nchini, akibainisha kuwa maafisa wa madawati hayo ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Zainab Katimba, alisema halmashauri za wilaya zinapaswa kuweka utaratibu wa kuwawezesha maafisa wa madawati ya msaada wa kisheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, ikiwemo kuwapatia rasilimali na ushirikiano unaohitajika.
Alisema kwa sasa wapo maafisa 446 wa madawati ya msaada wa kisheria katika halmashauri mbalimbali nchini wanaoendelea kutoa huduma hizo, huku akisisitiza kuwa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya halmashauri, wizara na wadau wa huduma za kisheria kutapanua zaidi wigo wa upatikanaji wa haki kwa wananchi.





SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.