Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo wanatakiwa kuhakikisha wanatenga na kuanzisha ofisi za Chama cha Watu Wenye Ualbino (TAS) katika maeneo yao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Dkt. Mganga ametoa maagizo hayo leo Novemba 27, 2025, wakati alipotembelea na kukagua ofisi mpya ya TAS iliyopo katika Manispaa ya Singida, ambapo amesisitiza kuwa uwepo wa ofisi hizo utasaidia kuimarisha uratibu, ulinzi na maendeleo ya kundi hilo.

Amesema kuanzishwa kwa ofisi hizo kunatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika ustawi wa watu wenye ualbino, kwa kuwa zitakuwa kiungo muhimu cha kuwahudumia kupitia ushauri wa kiafya, upatikanaji wa vifaa kinga vya ngozi, miwani maalum na mafunzo ya kujikinga na madhara ya jua.Kadhalika Kupitia huduma hizo, watu wenye ualbino wanatarajiwa kupata nafasi bora ya kujilinda dhidi ya saratani ya ngozi na matatizo ya macho ambayo yamekuwa changamoto kwao kwa muda mrefu.
Aidha, Dkt. Mganga amesema uwepo wa ofisi za TAS katika halmashauri mbalimbali utachangia kupunguza unyanyapaa na ukatili kwa sababu zitakuwa chombo muhimu cha kuendesha kampeni za uhamasishaji na kutoa elimu kwa jamii kuhusu ualbino. Ametaja kuwa ofisi hizo pia zitatoa fursa za kiuchumi kwa watu wenye ualbino kupitia mafunzo ya ujasiriamali, stadi za kazi na kuwaunganisha na miradi ya maendeleo itakayowanufaisha moja kwa moja.
Ameongeza kuwa ofisi hizo zitasaidia kukusanya takwimu sahihi kuhusu mahitaji na changamoto za watu wenye ualbino, hali itakayowezesha serikali na wadau kupanga mipango na kuelekeza rasilimali kwa ufanisi zaidi. Vilevile, ofisi hizo zinatarajiwa kuwa sehemu salama ya kutoa taarifa za vitisho na kupokea msaada wa kisheria au ulinzi wa haraka pale inapohitajika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Singida ameishukuru serikali ya mkoa kwa kuwezesha kupatikana kwa ofisi hiyo, akisema itakuwa kitovu cha uratibu na daraja rasmi litakalowaunganisha watu wenye ualbino kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa. Amesema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ushiriki wa kundi hilo katika shughuli za maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine wanaojihusisha na masuala ya watu wenye ualbino.

SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.