Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Singida,Mheshimiwa Halima Dendego,amekabidhi msaada wa vyakula na vinywaji kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Eid El-Fitr.
Vituo vilivyonufaika na msaada huo ni Thanaratul-Qadiria, kinachoongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issah Nassoro, kilichopo mtaa wa Majengo, pamoja na kituo cha Malaika wa Matumaini kinachoendeshwa na Kanisa Katoliki, Jimbo la Singida, huku msaada huo ukiwa na thamani ya jumla ya Shilingi milioni tano.
Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema Dk. Samia ametoa mchango huo kama ishara ya mshikamano na upendo kwa watoto hao, ili nao wajione sehemu ya jamii kama watoto wengine wanaoishi na familia zao.
"Rais ameona umuhimu wa kushiriki na ninyi katika furaha ya Sikukuu ya Eid, ili msijisikie wapweke.. hili ni jukumu letu sote kama jamii kuhakikisha mnapata malezi bora na faraja tele ya maisha," alisema Dendego.
Aidha, aliwataka wadau wa maendeleo na watu wenye mapenzi mema, kujitokeza zaidi kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, ili kuhakikisha wanawalea na kiwaweka kwenye mazingira bora, yanayowapa matumaini ya maisha thabiti, ya baadaye.
Msaada uliotolewa katika vituo hivyo ni mchele, mafuta ya kupikia, sukari, sabuni, vinywaji baridi, maji pamoja na mbuzi wanane, watakaotumika kwa ajili ya kitoweo cha Sikukuu ya Eid El-Fitr.
Viongozi wa vituo hivyo, akiweno sheikh wa Mkoa wa Singida Issah Nassoro, walishukuru kwa msaada huo, wakieleza kwamba utasaidia kuboresha lishe na furaha ya watoto waliopo katika vituo vyao.
Akizungumza baada ya tukio mtoto Nasibu Waziri, kwa niaba ya watoto waliopokea msaada huo ameonyesha furaha na kumshukuru Rais Samia kwa upendo wake, huku akiahidi kuwa watakua wakimwombea kwa Dua, na kuendelea kusoma kwa bidii ili kufanikisha ndoto zao za baadaye.
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni kipindi ambacho waumini wa dini ya Kiislamu hutumia kufanya ibada, kutafakari na kusaidiana, ili kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu pamoja na jamii inayowazunguka.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.