Madereva wa vyomo vya moto hasa bajaji na bodaboda wamewahimizwa kujiunga na chuo kikuu huria ili waweze kujiendeleza kielimu na kuboresha huduma zao, ambapo kwa kufanya hivyo watasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa wito huo juzi wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yaliyofanyika kwenye kituo cha zamani cha mabasi cha Mjini Singida.
Amesema masomo ya chuo kikuu huria humwezesha mtu kujiendelea kwa kupata elimu bora bila kuathiri shughuli zake za kila siku hasa za kujipatia kipato.
“Dereva wa bodaboda, bajaji au mkazi yeyote mkoani kwetu, tusiridhike na elimu tuliyonayo, kumbukeni elimu haina mwisho. Hivyo tutumie chuo chetu hiki cha huria kujiendeleza kielimu. Tukiwa na wasomi wengi mkoa wetu kwa vyovyote lengo la kuwa na uchumi wa kati na chini ya viwanda utalifikia kwa haraka”, amesema.
Dkt Nchimbi amwataka madereva wa vyombo vya moto kutii na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na sio tu kuendeshwa na kamera za barabarani.
“Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto, hawaheshimu kabisa sheria za usalama barabarani, wanaendeshwa na kamera. Siku moja yupo dereva mmoja wa bodaboda alikuwa mbele yangu, huku akiandika ujumbe kwenye simu yake. Utamaduni huu haufai kwa sababu ni chanzo cha ajali”,amesema Dkt.Nchimbi.
Aidha amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba kusimamia zoezi la madereva wa bajaji na bodaboda kujiunga na Chuo kikuu Huria.
“Hebu angalia uwezekano wa kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya madereva hawa kujiendeleza kielimu. Tunataka ifike siku tuwe na madereva hawa wana diploma au digrii, kwa hili nina imani na wewe utaweza kuwasaidia vizuri”, amesema.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema atagharamia safari ya viongozi wa madhehebu ya dini kwa kutoa kiasi cha shilingi laki tano, kwenda kufanya sala maalum kwenye maeneo yaliyokidhiri kwa vitendo vya ajali.
“Karibu kila wilaya ina eneo ambalo ajali haziishi kutokea mara kwa mara. Nina imani Mungu hajanipa mkoa wenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajali. Nimekubaliana na viongozi wangu wa madhehebu ya dini wataenda katika maeneo hayo, na kuomba Mungu atuondolee balaa la ajali za barabarani kwenye maeneo hayo”, amesema.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba amewaagiza viongozi wa madereva wa bodaboda na bajaji, kusimamia vema madereva hao ili wapunguze ajali za barabarani.
Mmoja kati ya wakazi wa Manispaa ya Singida, Njolo Kidimanda, amesema kuwa kuna haja serikali kuongeza kiwango cha faini kwa madai kiwango kilichopo, hakiwaogopeshi kabisa baadhi ya madereva.
Aidha, Kidimanda ameshauri madereva kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu salama, ili kusaidia majeruhi wa ajali barabarani wenye hitaji la damu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, jumla ya watu 68 wamefariki kutokana na ajali za barabarani kati ya Januari hadi Oktoba mwaka huu. Idadi hiyo imeonyesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani kwa kuwa katika kipindi hicho hicho mwaka jana, watu 152 walifariki.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.