Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego amezindua rasmi Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida leo tarehe 19 Mei, 2025 katika viwanja vya Stendi ya zamani Manispaa ya Singida.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni Rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Singida na kuja kuzindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa kuwa ni fursa kwa wananchi wa Mkoa huo kutatuliwa changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.
"Kipekee naishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa kunifikiria na kunipa wajibu huu mkubwa wa kuwa Mgeni Rasmi katika Halfa hii ya Uzinduzi wa Kamati na Kliniki ya Sheria bila malipo katika mkoa wetu”.Amesema Mhe. Dendego.
Mhe. Dendego amesema kuwa kuzinduliwa kwa Kamati hiyo pamoja na masuala mengine, kutasaidia Kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya Serikali, kuwawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria katika maeneo yao, Kuwawezesha Mawakili wa Serikali kushirikiana na wadau wengine katika kutatua kero za wananchi na kupunguza malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi.
“Naomba kukuahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa nitazisimamia Kamati hizi kikamilifu ili ziweze kuwa na tija katika mkoa wetu.” Amesema Mhe. Dendego
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Singida ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Sheria bila malipo ili waweze kupata huduma mbalimbali za kisheria hususani katika masuala ya mirathi, Ardhi, ndoa na Ajira.
"Nitoe wito kwa Wananchi wa Singida kujitokeza kwa wingi katika Kliniki hii kwani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuja na Wataalamu waliobobea katika masuala ya Kisheria na wanatoa huduma hii bure kabisa.”Amesema Mhe. Dendego
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa kuzinduliwa kwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Sheria kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida ni mojawapo ya hatua za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa moja ya njia inayotumiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajibika kwa wananchi ni kutoa ushauri na msaada wa kisheria kwa wananchi kwa kutumia Kamati za Ushauri wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa na ngazi za Wilaya.
"Lengo kuu la uanzishwaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya ni kurahisisha usimamizi wa utoaji wa ushauri wa kisheria kwa wananchi katika maeneo husika”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria kwa Mkoa wa Singida utafuatiwa na Kliniki ya sheria kuanzia tarehe 19 hadi 25 Mei, 2025 ambapo huduma za ushauri wa kisheria zitatolewa kwa wananchi bila malipo, ambapo amesisitiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itatoa huduma hizo kwa ubora.
Kliniki hiyo ya Sheria inalenga kusogeza huduma za sheria karibu na wananchi, kuwaongoza wananchi katika taratibu za kupata haki zao pale zinapovunjwa au zinapoonekana kuelekea kuvunjwa, kutoa elimu ya sheria kwa wananchi na kuongeza ushirikiano miongoni mwa Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea, na kuepusha au kupunguza mashauri yasiyo ya lazima.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.