Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida,Daktari Fatuma Mganga amewaasa wadau Kuendelea kuwajibika katika kuhakikisha usalama wa watoto,vijana na familia zinazoguswa na mradi wa USAID-Kizazi hodari kwa kupatiwa huduma stahiki kwa mafanikio chanya kwa mnufaika mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
Ameyasema hayo aliposhiriki katika kikao cha mrejesho wa mradi wa USAID,Kizazi hodari kanda ya kaskazini Mashariki chenye lengo la kutoa mrejesho wa utekelezaji wa mradi kwa mwaka 2024 katika Halmashauri nne, kujadili na kuweka mikakat ya utekelezaji wa shughuli za mradi kwa mwaka mpya 2025 na kutambulisha Halmashauri ya Itigi iliyoongezwa kwenye utekelezaji wa Mradi huo kwa mwaka wa fedha 2025.
"Tuna wajibu wa kuwafanya watoto wetu wawe salama, wenye furaha wakati wote kwa kuwapenda,kuwajali na kuhakikisha wanafikia ndoto zao wakiwa na uzalendo na kujivunia kuwa Watanzania.Tukatekeleze mradi huu kwa tija na ushirikiano katika kuhakikisha matokeo makubwa kwenye kuibua Watoto wote wanaohitaji huduma na kuhakikisha wote wanapatiwa huduma muhimu" alisema Daktari Fatuma Mganga.
Lengo la mradi huu ni kuboresha na kuimarisha Afya na Ustawi wa Watoto, Vijana na Kaya zao walioathiriwa /kuathirika na Virusi vya Ukimwi. Lengo likitegemea kufikiwa kwa huduma mbalimbali zinazotolewa na mradi huo ikiwemo afya, lishe, msaada wa kisaikolojia, ulinzi na usalama wa mtoto, uimarishaji uchumi wa kaya na elimu kupitia mfumo jumuishi wa kitaifa wa usimamizi wa Mashauri ya watoto.
Pia amepongeza uongozi wa makao makuu ya KKKT kwa kuendelea na utekelezaji wa mradi huo ambao Mkoa wa Singida ni sehemu ya wanufaika wa mradi huo katika wilaya za Ikungi, Manyoni, Iramba na Manispaa ya Singida .
Kwa mwaka wa fedha 2024 jumla ya walengwa 8,185 walifikiwa na kupewa huduma sawa na asilimia 119 ya 6,890 waliopangwa kufikiwa na kupewa huduma huku mwaka 2025 mradi ukipanga kuwafikia Jumla ya walengwa10,389 katika Halmashauri tano za mradi wenye kaulimbiu isemayo," Kizazi Hodari - Taifa Endelevu’"
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.