Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewataka madiwani wa Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Singida (DC) kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 100 pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato, ili kuimarisha ujenzi na ukarabati wa barabara pamoja na miundombinu mingine muhimu ya kijamii.
Mhe. Dendego ametoa wito huo leo Januari 15, 2026, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa Waheshimiwa Madiwani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, yakilenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika hafla ya ufungaji mafunzo hayo, Mhe. Dendego amesema madiwani wana wajibu mkubwa wa kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya halmashauri zao, akisisitiza kuwa mapato hayo ndiyo nguzo ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Ukusanyaji wa mapato unatakiwa uwe wa asilimia 100. Ninyi madiwani ndiyo mnatakiwa kusimamia upatikanaji wa mapato haya, kwa kuwa ndiyo yanayosaidia ujenzi wa barabara, madarasa na miundombinu mingine muhimu. Haitakiwi kuwaambia wananchi wasilipe kodi; kodi hizi ni kwa maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mhe. Dendego amewataka madiwani kuhakikisha usajili wa wanafunzi unafanyika kwa asilimia 100 katika kata zao, hususan kwa watoto wenye sifa za kuanza shule, na kusimamia kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni kwa wakati.
Aidha, amewakumbusha madiwani kuendelea kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi, akisisitiza kuwa jukumu lao la msingi ni kuwahudumia wananchi na kusimamia maendeleo katika maeneo yao.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza Januari 13 hadi 15,2026 yalilenga kuwajengea uwezo madiwani katika masuala ya uongozi, usimamizi wa mapato, na uwajibikaji kwa jamii wanazoziongoza.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.