Mkoa wa Singida umepokea magari matano yenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni795 kwa matumizi katika Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Singida kwa ajili ya kusimamia shughuli za sekta ya maji.
Magari hayo yamekabidhiwa leo (Novemba 6, 2024) na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ni kwa ajili ya Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira katika Wilaya za Singida mjini,Manyoni na Kiomboi, RUWASA Mkoa wa Singida na RUWASA Wilaya ya Iramba.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida, Lucas Said, amesema magari hayo yametolewa ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kwamba mamlaka hiyo zinasaidia kutatua kero za maji katika Mkoa wa Singida.
"Kama unavyofahamu tunaendelea kufanya kazi kuhakikisha kwamba tunafikia malengo ya kufikia asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95 ifikapo Disemba 2025,tunaendelea na jitihada ili kufikia malengo haya ambayo ni pamoja na kupata vitendea kazi ili viweze kusimamia miradi ipasavyo," amesema Said.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA),Sebastian Warioba, amesema baada ya kukabidhiwa magari hayo watahakikisha wanafikia malengo ya kufikisha maji kwa wananchi kama ambavyo imeainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Sisi watumishi wa sekta ya maji katika Mkoa wa Singida tunakuahidi tutaendelea kuchapa kazi kwa umoja,uadilifu na kujituma ili tuweze kufikia yale malengo ambayo yameainishwa kwenye ilani ya CCM,tunatoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa namna wanavyotujari na kutusimamia katika kuhakikisha tunamtua ndoo mama kichwani," amesema Warioba
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dendego,amesema kiwango cha upatikanaji wa maji kwa sasa kimefikia asilimia 68.2 vijijini na asilimia 86 mjini hivyo bado hakijafikia kwenye malengo ya ilani ya CCM.
"Kupewa magari haya tumeongezewa mwendo,tumeongezewa kasi na ari kuhakikisha ile miradi yetu tunayotekeleza sasa iweze kutekelezwa kwa kasi kubwa ili kufikia malengo yaliyopo kwenye ilani ya CCM kabla ya muda uliopagwa," amesema.
Dendego amesema Mkoa wa Singida umejiwekea malengo ikifika Juni 2025 malengo ya kufikia asilimia 85 kupeleka maji vijijini na asilimia 95 mjini yatakuwa yamefikiwa.
Amesema serikali chini ya Wizara ya Maji imekuwa ikiendesha kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani hivyo ili kufanikisha kampeni hiyo ni lazima kuwepo na vitendea kazi kama magari.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.