Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa leo ameweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya cha Iglansoni kilichopo Kata ya Iglansoni Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida kilichogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 500.
Akiwahutubia Wananchi wa vijiji vya Iglansoni na Mnyange Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa fedha hizo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM lengo likiwa ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuleta unafuu wa maisha.
Akiwa katika ziara hiyo yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo amewataka viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani kuhakikisha wanatembelea na kuwasikiliza wananchi ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Aidha amewashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonesha katika ujenzi wa Kituo hicho ambapo waliweza kuchangia vitu mbalimbali pamoja na ulinzi wa vifaa vya ujenzi huo.
Amesema Serikali imeleta Milioni 350 kwa ajili ya maji ambapo watafiti walikumbana na changamoto ya upatikanaji wa chanzo cha maji kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wakazi wa Iglansoni hivyo kuwataka wananchi hao kuhifadhi mazingira kwa faida yao.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka viongozi kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo ili thamani ya fedha iliyotumika iweze kuonekana.
Waziri Mkuu amesema kuwa kazi mbili zilizobaki ni za korido kwenda kwa ajili ya kivuko na njia ya kwenda majengo mbalimbali pamoja na jengo la wodi ya wanaume na wanawake ambapo amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuleta Milino 250 kwa ajili ya kumalizia kazi hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akatumia muda huo kuwasisitiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya ili waweze kutibiwa kwa urahisi zaidi.
RC Serukamba amesema uwepo wa vituo hivyo vya Afya ni jitihada za Serikali kuleta huduma karibu na watu hivyo jitihada zozote zitatumika kuhakikisha kila mwananchi anapata Bima.
Naye Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde amesema wamejipanga kujenga vituo vya Afya 234 nchi nzima Ikungi ikiwemo na tayari fedha zishapelekwa, Serikali imeagiza magari ya kusafirishia wagonjwa ambapo Ikungi nayo watapata kwenye sehemu zenye mahitaji makubwa.
Hata hivyo Silinde ameendelea kusema kwamba Serikali imetoa Bilioni 13 Mkoani Singida kwa ajili ya ujenzi wa shule ambapo madarasa 667 yamejengwa na wanafunzi wanaendelea na shule.
Aidha Serikali pia imetoa Bilioni Tatu (3) katika mkoa wa Singida ili kujenga shule ya wasichana ambayo itachukua wanafunzi zaidi ya 1000.
Amesema Serikali imeendelea kutoa fedha Mkoani hapo kwamba bajeti ya Barabara imeongezewa kutoka Bilioni Tano (5) mwaka 2020 mpaka kufikia Bilioni 22 ili kuboresha na kufungua barabara mpya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi Justice Kijazi akitoa taarifa yake amesema Kituo hicho kimegharimu jumla ya Milioni 500 ambazo zilikuja kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zilikuja Milioni 250 mwezi Novemba 2021 na Milioni 250 zilikuja mwezi Mei 2022.
Amesema fedha hizo zilizotokana na tozo zimewasaidi wananchi wapatao 13,0608 kutoka katika Kijiji cha Iglansoni na Mnyange ambao walikuwa wakitumia zaidi ya km 60 kufuata huduma za Afya.
Waziri Mkuu pia ametembelea Hospitali ya wilaya ya Ikungi ambapo amewataka viongozi wa Wilaya hiyo kuharakisha umaliziaji wa majengo hayo ili yaweze kutumika kwa haraka.
Hata hivyo Waziri Mkuu alitembelea Ujenzi wa Chuo cha VETA Wilayani Ikungi ambapo amesema uwepo wa chuo hicho itawasaidia wananchi kupata elimu ya ufundi ambapo wataweza kujiajiri badala ya kusubiria ajira za Serikali.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.