Maonesho ya Saba ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji yamefunguliwa rasmi mkoani Singida na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi, ambapo katika hotuba yake amesisitiza umuhimu wa elimu ya kujitegemea huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kujifunza kupitia maonesho hayo ili kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza (Septemba 10, 2024) kwenye hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo Waziri Lukuvi amewasihi wananchi wa Singida na maeneo ya jirani kutumia fursa hii kujifunza na kuimarisha biashara zao kwa lengo la kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.
“Serikali imewaletea elimu ya kujitegemea, jitokezeni kujifunza kupitia maonesho haya ili kujikwamua kiuchumi. Mfanyabiashara mdogo jifunze kuwa mkubwa…., nawasihi muulize maswali na msubutu,” amesema Waziri Lukuvi.
Asisitiza kuwa, maonesho hayo ni fursa adhimu kwa wananchi, wajasiriamali, na vikundi mbalimbali kujifunza kuhusu fursa za uwezeshaji, kupata elimu ya kifedha, na kujionea bidhaa na huduma mbalimbali kutoka mifuko na taasisi zinazowezesha wananchi ambapo kutakuwa na bidhaa za wajasiriamali, semina za ujasiriamali uboreshaji wa biashara na ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu.
Akitoa salamu za Mkoa wa Singida, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Halima Dendego amekiri kuwa mmoja wa mashuhuda wa hatua za Serikali inazochukua ili kuwawezesha wananchi kiuchumi hususan katika wa Singida.
" Hakuna asiyejua au kufaidika na elimu bila malipo, ruzuku za mbolea, viuatilifu na mbegu bora za alizeti, umeme vijijini, zahanati vijijini, vituo vya afya na mahospitali yenye vifaa tiba vya kisasa kabisha, wataalamu bobezi, na dawa muhimu, huduma za maji safi na salama, mabarabara, vivuko, madaraja yanayojengwa" Amesema RC. Dendego
Amesema pia kupitia fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi chini ya program ya kuzifikia kaya zisizojiweza, yaani TASAF, umewezesha kufikiwa kwa zaidi ya kaya 58,000 huku fedha zaidi ya shs. 22 bilioni zikitumika.
Amesisitiza kuwa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu zimetolewa huku shs. 2.5 bilioni kutengwa kwa ajili ya walengwa, aidha vikundi 7 vya vijana kufaidika na fedha za mfuko wa vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
RC. Dendego amesema kwamba maonyesho haya yanakuja kuongeza kasi ya kuziangazia fursa za kiuwezeshaji na kama mkoa wa Singida watahakikisha kuwa wanatumia fursa zilizopo za ndani na nje ili kuendelea kukuza uchumi wa mkoa na wananchi wake huku akitoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo.
Naye, Katibu Mkuu wa baraza la Taifa la uwezeshaji (NEEC) Bi. Bein'g Issa amesema, kuongezeka kwa hamasa ya wananchi kutafuta vigezo vya kukopesheka pamoja na kujiunga kwenye vikundi vya kiuchumi kama SACCOS na VICOBA itawakutanisha wajasiriamali na watoa huduma mbalimbali wa Serikali na binafsi watakaosaidia kuongeza thamani na kukuza biashara zao.
Bi. Being amesema, wana mategemeo ya kuwa na shughuli za kutangaza fursa za mifuko hiyo pamoja na Taasisi nyingine wezeshi, kutoa mikopo kwa wajasiriamali, kuuza bidhaa za wajasiriamali pamoja na kutoa mafunzo ya uendelezaji biashara kwa wajasiriamali.
"Mpaka sasa Baraza linaratibu jumla ya Mifuko ya Uwezeshaji na Programu 72 ambayo 62 ipo Serikalini na 10 ipo Sekta binafsi, hivyo lengo kuu la Maonesho haya ni kutoa uelewa wa fursa za Mifuko kwa Wananchi ambapo ilionekana mifuko mingi haifahamiki kwa wananchi hivyo kuchelewesha kufikisha huduma za uwezeshaji kwa wananchi" Bi.Bein'g.
Maonesho hayo yanatarajiwa kuendelea kwa siku saba ambapo kilele ni tarehe 14 Septemba, 2024.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.