Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Halima Dendego, amewagiza viongozi wote mkoani hapa kuhakikisha kila mmoja anakuwa na shamba ili wananchi wajifunze kwao badala ya kuwahimiza walime ilhali hawajihusishi na kilimo.
Ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha kupata taarifa kuhusu mgao wa mbegu za alizeti zenye ruzuku zilizoletwa mkoani Singida ambacho kiliwashirikisha wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri,wenyeviti wa halmashauri na maafisa kilimo.
"Tusiwe tunaimba wimbo wa kilimo wakati sisi wenyewe hatulimi, tukubaliane hapa kuanzia mkoani,wilayani hadi kwenye kata kila mmoja angalau awe na shamba la ekari moja litakuwa ni shamba darasa kwa wananchi kufika kujifunza ili waone mbolea na mbegu zinavyofanya kazi," alisema.
Mhe.Dendego ameagiza mbegu za alizeti zilizoletwa mkoani Singida zikishafika wilayani zisambazwe haraka kwa wakulima ili kilimo cha zao hilo kiweze kuanza mara moja.
Amesema viongozi wa Wilaya zote waendelee kuwahamasisha wananchi kulima ili kuwango cha uzalishaji wa alizeti kiongezeke katika msimu huu wa kilimo kwani Mkoa wa Singida unategemewa kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti.
Mkuu wa Mkoa alisema katika msimu wa kilimo mwaka huu, Mkoa umepanga kulima ekari 1,025,641 za alizeti na kupata mavuno tani 1,000,000.
Mhe.Dendego amesema kulingana na ekari hizo zinazotarajia kulimwa kunahitajika mbegu za alizeti tani 2051 ambapo mpaka sasa kwenye halmashauri kuna tani 101.814 mbegu za alizeti
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga ameiomba Serikali iangalie namna ya kulegeza masharti ili wananchi ambao hawana fedha taslimu wakopeshwe na waje walipe baada ya kuvuna mazao.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.