Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, leo amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ndani ya Manispaa ya Singida, ambapo alipata fursa ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka unaotekelezwa katika eneo la Manga, Kata ya Mtipa.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mganga sambamba na timu ya ufuatiliaji ya Mkoa walisomewa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa na wa kimkakati, ambao unalenga kuboresha huduma za usafi wa mazingira na afya ya umma kwa wakazi zaidi ya laki moja wa Manispaa ya Singida.
Mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), na unahusisha ujenzi wa mabwawa matano ya kutibu majitaka kwa teknolojia ya kisasa (anaerobic, facultative & wetlands), pamoja na maabara ya kupima ubora wa majitaka yaliyotibiwa, gari la kubeba majitaka, barabara na uzio wa kuzunguka eneo la mradi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi kufikia Septemba 2025, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 71, huku mabwawa yote matano yakiwa tayari yamekamilika. Shughuli zinazoendelea ni pamoja na ulazaji wa mabomba ya kuunganisha mabwawa, ukamilishaji wa jengo la maabara, jengo la mlinzi na usimikaji wa nguzo za fensi.
Mradi ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 16 Mei 2023, na unatarajiwa kukamilika tarehe 27 Oktoba 2025, kwa kipindi cha miezi 29 na siku 11.
Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa zaidi ya wananchi 112,934 watanufaika moja kwa moja na mradi huo kwa kupata huduma bora za usafi wa mazingira. Aidha, mradi huo unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kuenea kwa magonjwa ya tumbo na kuhara yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na utiririshaji wa majitaka usio rasmi.
Majitaka yaliyotibiwa yatatumika kwenye kilimo cha mboga mboga na matunda, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wa maeneo ya jirani. Vilevile, mradi unazalisha mbolea bora ya muda mrefu ambayo itapatikana kutoka kwenye mabwawa hayo, na inakadiriwa kudumu shambani kwa hadi miaka mitatu.
Zaidi ya hayo, eneo la mradi lina ukubwa wa meta za mraba 211,005, ambalo litahifadhiwa na kuendelezwa kwa upandaji miti na uboreshaji wa uoto wa asili, hatua itakayochangia kuimarisha hali ya hewa ya eneo hilo.
Dkt. Fatuma Mganga amepongeza hatua kubwa ya utekelezaji iliyofikiwa na kueleza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.