Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Halima Dendego amewaasa waumini kutumia vizuri majukwaa ya kanisani katika kuhakikisha amani inadumishwa na sio kuleta uchochezi na kuhamasisha vurugu ambayo matokeo yake husababisha ukosefu wa amani.
Ameyasema hayo leo Septemba 21,2025 katika kanisa la Uweza wa Bwana kata ya Minga akiwa kama Mgeni rasmi katika kongamano maalum la kuombea amani kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Amesema kuwa waumini wanapaswa kujifunza na kujitahadhari kwa kutumia mifano ya nchi za jirani ambazo hazina amani kutokana na kukosa utulivu wa kisiasa ambao unapelekea wananchi kushindwa kujihusisha na shughuli za kiuchumi na uzalishaji mali ambazo hupelekea kukosa vyakula na kukumbwa na baa la njaa na vifo vingi.
"Amani katika Taifa ndiyo msingi wa kila kitu,hakuna maendeleo wala shughuli za kiuchumi bila amani,amani ikikosekana hakuna usalama,hatutoweza kuabudu wala kutafuta riziki.Hatuna Taifa lingine la kukimbilia bali sisi Tanzania ndio Taifa ndio kimbilio la wengine waliopoteza amani.
Hivyo ameiasa jamii kuikumbatia amani iliyopo bila kufuatisha maneno na msukumo wa watu mbalimbali wenye nia ovu ya kuharibu amani iliyopo kwa kutumia majukwaa ya kisiasa hususani katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
"Ili kumaliza migogoro yote na kuitunza amani yetu iliyopo tusikubali kuwasililiza wale wote wanaoshawishi wananchi kutoshiriki katika uchaguzi mkuu mwaka huu.ili kuweza kuchagua viongozi bora wanaoona wanafaa kwenda kuwasilisha mapendekezo na mahitaji yao Bungeni ni muhimu na haki yako kikatiba kushiriki zoezi la kupiga kura ifikapo siku ya Uchaguzi."amesema Mhe.Dendego.
Mhe.Dendego amehitimisha kwa kusema kuwa Serikali yetu haina dini bali inawaongoza wananchi ambao wana dini zao hivyo amewaomba waumini hao kuungana kufanya maombi kama hayo kwani suala la amani ya nchi ni jukumu la kila mmoja wetu.
Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Uweza wa Bwana Mch.Barick Mapigano, amewaasa waumini kwenda kuwachagua Viongozi bora ambao ni Watumishi kutoka kwa Mungu ili kwenda kuwa Watumishi kwa wananchi kila mmoja kwa nafasi yake wakiwemo Madiwani,Wabunge na Rais kwani uchaguzi ni jambo jema ambalo huondoa malalamiko baina ya watu,fadhaa na kukata tamaa kwani kupiga kura ni agizo kutoka kwa Mungu.
Kadhalika amewataka Wachungaji na waumini wengine kuhakikisha hawakati tamaa ya kuhubiri amani kuelekea uchaguzi kwa kuhofia kupewa majina mabaya akisisitiza kuwa jambo jema zaidi ni amani na sio kuogopa kuihubiri amani na utulivu kwani endapo amani ikitoweka nafasi ya kuhubiri wala kusikiliza mahibiri haitapatikana hivyo tuidumishe amani tuliyonayo na tusichoke kuwasisitiza wenzetu kuidumisha
Akizungumza baada ya ibada,Bi.Miriam Israel amesema leo ni siku muhimu sana kwani ni ibada njema inayohubiri amani kwa nchi ya Tanzania na anaitumia siku hii na zile zijazo kuwahimiza waumini na wanajamii wenzake kuhakikisha wanashiriki uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2025 sambamba na kuhudhuria kampeni zinazoendelea ili kuweza kusikiliza sera mbalimbali za wagombea hao ili kuchagua zinazowagusa wananchi na kuwaletea maendeleo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.