Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ameagiza kuundwa kwa Kamati ya wataalamu wa ardhi kutoka halmashauri za Mkalama na Singida Vijijini ili kutatua mgogoro wa shamba la Serikali lililopo katika Kijiji cha Mpambaa lengo likiwa kuondoa adha wanazozipata wananchi wa maeneo hayo.
Dkt. Mahenge ametoa maelekezo hayo Aprili 3, 2022 mara baada ya kukutana na watendaji wa halmashauri hizo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kusikiliza malalamiko ya pande zote mbili kwa lengo la kupata utatuzi zaidi wa mgogoro unaoendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza wakati wa kikao hicho
Akipokea taarifa kutoka pande mbili za mgogoro imeelezwa kwamba umekuwa na uharibifu wa mazao kutokana na kuliwa na mifugo katika mashamba hayo ambayo imekuwa ikisababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Wakati huo wafugaji nao wakilalamikia zoezi la ukamataji wa mifugo ambayo mingine ilipigwa mnada baada ya kukamatwa ikiwa inaharibu mazao hayo.
Kutokana na vitendo hivyo RC Mahenge akasisitiza uundwaji wa kamati hiyo kwa haraka na kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia haki kanuni sheria pia kamati ihakikishe inashirikisha wananchi wa maeneo husika.
Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho Dkt. Mahenge akawasisitiza viongozi hao kutokuwa chanzo cha migogoro bali kwenda kuwasihi wananchi wao kuendelea kuwa na uvumilivu wakati serikali inaendelea na taratibu za kitaalamu ambazo zitakamilika kabla ya msimu ujao wa kilimo.
Akimalizia mazungumzo yake Mkuu wa Mkoa huo amesema kwa kuwa msimu huu shughuli za kilimo na kiuchumi zilishaanza katika shamba hilo hivyo ziendelee kama kawaida hadi hapo timu ya wataalamu iliyoundwa itakapokamilisha zoezi lake na kutoa taarifa ndipo tamko rasmi litatolewa na serikali ya Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akizungumza wakati wa kikao hicho
Awali akielezea mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili aliunga mkono uundwaji wa kamati hiyo ambapo amesema sababu ya mgogoro huo sio wananchi bali ni baadhi ya viongozi pamoja na wataalamu waliohusika na masuala ya upimaji ardhi.
Hata hivyo Dc Muragili alisema Halmashauri ya Singida Dc ilianza kulisimamia shamba hilo takribani miaka 23 kuanzia mwaka 1999 hadi leo 2022.
“Sisi sote ni ndugu, Viongozi tukae na wataalamu ili kuziangalia kwa kina GN zilizotumika kupata mipaka ya maeneo ya pande zote ili tuweze kukubaliana. Swala la mpaka ni tamko tuu hivyo nashauri tutatue kwanza tatizo la GN”. Alisema Mhandisi Muragili
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akizungumza wakati wa kikao hicho
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amesema alipokea historia ya shamba hilo kutoka kwa mwananchi wake anayeishi jirani na shamba hilo ambapo alielezwa kuwa hapo awali shamba hilo lilikuwa likisimamiwa na serikali ya mkoa kwa shughuli za mradi wa uzalishaji mbegu za Mtama, Alizeti, Mahindi na mazao mengine.
Alielezwa kuwa mara baada ya mradi huo kusitishwa baadhi ya wananchi wa kijiji cha jirani na shamba wakaanza kulitumia kwa shughuli za kilimo ili kujikwamua kiuchumi. Baada ya kupokea historia hiyo Mkuu wa Wilaya huyo aliamua kutuma timu ya wataalamu wa ardhi ili kutambua mipaka ya pande hizo ambapo ikabainika changamoto ni vifaa vilivyotumika kutambua mipaka kuwa hazitoi taarifa zinazofanana.
Akizungumza kwenye kikao hicho Sophia Kizigo alisema wananchi wa upande wa Mkalama wanasubiri kusikia tamko la serikali ya Mkoa kuhusu suluhisho la mgogoro huku akisisitiza weledi na utaalamu ufanyike katika zoezi hilo ili kupata utambuzi wa mipaka hiyo kwa usahihi na si kufuata kihistoria.
Kikao hicho kilihitishwa na Mkuu wa Mkoa huo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko, Wakuu wa Wilaya ya Singida Dc na Mkalama, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri za wilaya husika, Wabunge, watendaji wa halmashauri ya Singida Dc na Mkalama pamoja na wananchi wanaoishi jirani na shamba hilo.
kikao kikiendelea
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.