Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge amewapongeza wakandarasi wanaosimamia miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi na ofisi za wakuu wa Wilaya ikiwemo Ikungi, Singida DC na Mkalama kwa hatua majengo hayo yalipofikia na kuwataka kukamilisha ndani ya kipindi kisichozindi siku 15 kazi hizo zilizobaki ziwe zimekamilika na ofisi kuanza kutumika.
Pongezi hizo amezitoa leo tarehe 31 Januari 2022 wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa ofisi hizo ikiwa ni pamoja na kuona changamoto zilizokabili ujenzi na kuzitafutia suluhisho kwa kipindi kifupi.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wilayani Mkalama Dkt Mahenge akawataka wakuu wa Idara ambao wanatakiwa kuzitumia nyumba hizo kuhakikisha wanaingia kabla ya tarehe 15 na endapo atakuwepo yeyote ambaye hatatekeleza agizo hilo kwa sababu zake hatalipwa posho ya nyumba kama inavyofanyika hivi sasa alibainisha RC Mahenge.
Aidha RC Mahenge ametoa siku mbili kwa wakandarasi wa nyumba za watumishi Mkalama kumalizia uwekaji wa vifaa vidogo vidogo vilivyobaki vikiwemo soket, Koki za maji na taa, endepo kutakuwa na changamoto ya umaliziaji huo kila mtumishi anayestahiki kuingia kwenye nyumba hizo akamilishe Mwenyewe.
Aidha akawakumbusha viongozi mbalimbali wa Wilaya hiyo kuhakikisha kwamba wanafuatilia kwa ukaribu ujenzi wa ofisi ya DC ambao umekuwa ukisuasua kwa kufanya mawasiliano na makao makuu ya Hazina kuhakikisha fedha zilizotolewa zinamfikia mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo nchini TBA.
Awali akitoa taarifa za ujenzi wa nyumba hizo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mkalama Asia Messos amesema ujenzi wa nyumba za watumishi umegharimu kiasi cha Tsh.milioni 401.2
Amesema mradi huu ukikamilika utaokoa kiasi cha Tsh. milioni 3.6 zinazotumika kila mwezi kulipa stahiki za wakuu wa Idara sita ambapo kwa sasa zitatumika kwa ajili ya kazi nyingine za maendeleo aliendelea kusema Mkurugenzi Mtendaji.
Akijibu baadhi ya changamoto zilizopo katika ujenzi huo RC Mahenge akamtaka meneja wa Shirika la umeme TANESCO kuhakikisha wanafikisha umeme katika nyumba hizo ndani ya siku tano ili majengo hayo yaanze kutumika.
Wakati huo huo Kaimu Meneja wa wakala wa majengo TBA Mkoa wa Singida Mhandisi Hadija Abdalah amesema mradi huo unagharimu kiasi cha Tsh, Bilion 1.2 na ulianza mwaka 2018 ambapo changamoto imekuwa ni upatikanaji wa fedha za mradi kwa wakati jambo lililosababisha kazi kusuasua ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 80.
Hata hivyo Mhandisi Hadija amesema kutokana na kuchelewa fedha kwa muda mrefu kumesababisha kupanda kwa gharama za manunuzi ya vifaa vya ujenzi pamoja na kuchelewa kufanyika kwa uchunguzi wa udongo (geotechnical investigation) kwa zaidi ya miezi mitano.
Akiendelea na ziara yake Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge akatembelea mradi wa ujenzi wa ofisi ya DC katika wilaya ya Singida vijijini ambapo kwa mujibu wa mtoa taarifa Kaimu Mkurugenzi Masomo Mbelwa amesema ujenzi umefikia asilimia 75 na linatarajiwa kukamili hivi karibuni.
Amebainisha kwamba zipo changamoto za upatikanaji wa umeme katika eneo hilo na kuadimika kwa saruji kutoka viwandani kulikosababishwa na utekelezaji wa miradi ya shule kupitia fedha za UVIKO19 pamoja na changamoto za miundombinu ya barabara katika eneo hilo.
Akimalizia ziara yake Wilayani Ikungie RC Mahenge akaendelea kuipongeza kampuni Tanzu ya Mzinga iliyoko chini ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa hatua nzuri waliyofikia katika ujenzi ambapo wametumia gharama za kampuni kukamilisha kazi hiyo kwa asilia 95.
Amewataka kuendelea kutumia mbinu walizozitumia awali ili kukamilisha kwa asilimia mia moja wakati Serikali ikiandaa mazingira ya kuweza kulipa fedha zote zilizotumika katika ujenzi huo.
Ziara hiyo iliwahusisha Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Makatibu Tawala wasaidizi, Wakurugenzi na wakuu wa Idara mbalimbali
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kutoka kushoto) akikagua moja kati ya nyumba 6 za wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Mkalama. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa Dorothly Mwaluko (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos mara baada ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkalama
Ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkalama ukiendelea
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Singida Vijijini mara baada ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika kijiji cha Mwahango
Muonekano wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika kijiji cha Mwahango
Mkuu wa Mkoa wa Singida akizungumza na viongozi mbalimbali wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa Mkuu wavWilaya ya Ikungi
Mkuu wa MKoa wa Singida (kushoto) akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya Ikungi
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothly Mwaluko akizungumza wakati wa ziara hiyo
Muonekano wa ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Ikungi unaotekelezwa na Kampuni Tanzu ya Mzinga - Morogoro
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.