MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, ameanza ziara ya siku 13 ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri za mkoa huu ambapo leo (Mei 16, 2023) ameanzia katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Katika miradi aliyoitembelea na kuikagua katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Serukamba amewagiza Watendaji kuhakikisha wanaisimamia ili iweze kukamilika kabla ya Juni 10, mwaka huu.
Miradi aliyoitembelea ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mugungia-Kaselya, ujenzi madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Muungano, ujenzi wa Zahanati ya Mugungia, ujenzi wa darasa moja katika Shule ya Msingi Mbelekese na ujenzi wa hosteli katika Shule ya Sekondari Mbelekese.
Miradi mingine ni ujenzi wa vyoo, jengo la mtoto, uzazi na miundombinu ya kuvunia maji ya kunawa mikono katika Zahanati ya Usure, ujenzi wa madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Luzilukulu, ujenzi wa bwalo la chakula na hosteli katika Shule ya Sekondari Ndago, kukagua ujenzi wa barabara ya Songambele-Misuna na ujenzi wa nyumba ya Afisa Tarafa ya Ndago.
Serukamba alihitimisha ziara yake siku ya kwanza katika Wilaya hiyo kwa kukagua ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Ulyang’ombe, ujenzi wa shule mpya ya mikondo miwili ya Ng’anguli, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya sekondari Kinampanda, ujenzi wa nyumba ya Afisa Tarafa Kinampanda, ujenzi wa madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Kitukutu na ujenzi wa zahanati ya Ulemo.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Ng’anguli, Mkuu wa Mkoa alisema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kumwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha anafuatilia kwa karibu mradi huo ili uweze kukamilika kabla ya Juni 10, mwaka huu.
Serukamba alimwambia Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Juvena Sebastian kama hawezi kusimamia ujenzi wa mradi huo na kukamilika haraka kabla ya Juni 10 amweleze Mkurugenzi mapema ili nafasi hiyo apewe mtu mwingine atakayeweza kusimamia ukamilike kwa haraka.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.